#HABARI: Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, ametoa rai kwa Majaji wa Mahakama Kuu nchini kuwa, namna watakavyotimiza wajibu wao ipasavyo katika utatuzi wa migogoro ya Mashauri yanayotokana na uchaguzi inaweza kuwa fursa mojawapo ya kurejesha imani ya umma kwa Mahakama.
Akitoa neno fupi la utangulizi wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mafunzo ya Namna Bora ya Uendeshaji wa Mashauri ya Uchaguzi yanayotolewa kwa Majaji wa Mahakama Kuu kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania Jijini Dodoma, Mhe. Dkt. Siyani amesema kuwa, katika jamii kuna baadhi ya watu hawana imani na taasisi mbalimbali za Umma ikiwemo Mahakama, ambapo malalamiko mengi yanahusishwa na huduma zinazotolewa.
Amesisitiza kwamba Mahakama ndio Chombo pekee chenye kauli ya mwisho kwenye utoaji haki kwa mujibu wa Ibara ya 107 A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa msingi huo Mahakama inayo wajibu wa kupokea, kusikiliza na kutoa maamuzi kwenye migogoro inayotokana na uchaguzi.
Amesema kwamba, uchaguzi ni mchakato unaohusisha ushindani baina ya watu kutoka kwenye vyama tofauti tofauti vya kisiasa, migororo inayotokana na ushindani huo imekuwa ikisababisha mashauri hayo kuwa na mvuto wa aina yake kwa umma, ni kwa msingi huo matarajio ya wananchi kwa Mahakama huwa ni makubwa.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yamelenga kubadilishana uzoefu juu ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu, Naibu Wasajili na Mahakimu Wafawidhi wa ngazi zote na hivyo kujengeana uwezo wa jinsi ya kushughulikia mashauri ya aina hiyo.
Mhe. Dkt. Siyani ameongeza kuwa mafunzo hayo ni fursa muhimu kwa Majaji ambao waliteuliwa baada ya chaguzi zilizopita kujua changamoto zinazojitokeza katika uendeshaji wa mashauri yanayotokana na chaguzi hizo, kufahamu kwa kina sheria za sasa za uchaguzi na usimamizi wa mashauri hayo.
#ITVDigital #ITVUpdates #ITVTanzania
#Follow @itvtz @radioonetanzania
@capitaldigitaltanzania