Marekani. Wanapozungumziwa wasanii wa muziki laini duniani jina la Kenny G, mpiga saxophone lazima liwepo.
Msanii huyu alizaliwa mwaka 1956 huko Seattle, Marekani watu wengi wamemfahamu kupitia nyimbo zake kama Songbird, Silhouette na Forever in Love. Nyimbo ambazo hazijawekwa maneno yoyote lakini hugusa mioyo ya watu kwa namna tofauti.
Kenny G alianza safari ya muziki akiwa na umri wa miaka 10, kwa kupiga saxophone katika redio za miji, akiwa kijana mdogo. Alijitosa kwenye muziki wa jazz na baadaye akaungana na bendi kadhaa kabla ya kuanza kazi yake binafsi miaka ya 1980.

Albamu yake ya Duotones ya mwaka 1986 ilimpa umaarufu mkubwa, hasa kutokana na wimbo “Songbird” uliopenya kwenye redio mbalimbali Africa Mashariki, Marekani, Asia na duniani kote.
Kwa sasa, muziki wa Kenny G umekuwa ukiheshimiwa na kuchezwa katika sherehe mbalimbali hasa wakati wa chakula. Hii ni kutokana na nyimbo hizo kuwafanya watu wajisikie wapo sehemu salama na ya kifahari. Kwa Bongo wapenda msosi wakisikia kianda cha wimbo wa “Going Home” au “Forever in Love” hukimbilia kupanga mstari ili wasipitwe.
Aidha kupitia mahojiano yake mbalimbali aliyowahi kuyafanya na vyombo vya habari kama CNN, Rolling Stone, na NPR (National Public Radio) ameleeza kwanini anatoa nyimbo zenye utulivu huku akiweka wazi kuwa lengo lake kubwa ni kutoa nyimbo zitakazogusa hisia za watu na sio kushindana na wasanii wengine.

“Mimi hupenda muziki unaoweza kufanya mtu apumue, afikirie mema, na ajihisi salama. Dunia ina kelele nyingi, kwa hiyo napenda kutumia saxophone yangu kama njia ya kutoa utulivu. Wakati napiga saxophone, sipigi noti tu napiga hisia. Nataka mtu akisikiliza wimbo wangu, ajisikie kana kwamba anaongea na moyo wake mwenyewe.
“Sijawahi kuona muziki kama ushindani. Wapo wapiga saxophone bora kuliko mimi, lakini mimi nachagua kufanya kitu kinachogusa moyo. Sio lazima uwe wa haraka au wa kelele ili uwe mzuri. Wimbo wangu unaweza kucheza harusini au hospitalini, lakini hisia zinabaki zilezile amani,”alisema Kenny
Kupitia muziki wake wa smooth jazz, Kenny G amepata mafanikio mbalimbali ikiwemo kuuza nakala milioni 75 za albamu duniani kote, jambo lililomfanya kuwa mpiga saxophone aliyeuza nakala zaidi katika historia ya muziki huo.

Albamu yake Breathless ya mwaka 1992 ndiyo iliyompa mafanikio makubwa zaidi, ikiuza zaidi ya milioni 15, huku wimbo wake wa Forever in Love ikimpatia Tuzo ya Grammy mwaka 1994 katika kipengele cha “Best Instrumental Composition.”
Mbali na Grammy, Kenny G amenyakuwa tuzo kadhaa kama American Music Awards, Soul Train Music Award, na Echo Award kutoka Ujerumani. Pia amewahi kuingia katika vitabu vya Rekodi za Dunia (Guinness World Records) baada ya kushikilia noti moja ya saxophone kwa zaidi ya dakika 45 mfululizo.
Kwa sasa, Kenny G ambaye ana zaidi ya miaka 60 anaendelea na shughuli zake za muziki akiwa nchini Marekani, ambako anaishi katika eneo la Malibu, California, huku akijiandaa na ziara yake ya kimataifa iitwayo “Miracles Holiday and Hits Tour 2025”. Ziara ambayo atatembelea miji kama Thailand, Malaysia, Ufilipino na sehemu nyingine.