
Chanzo cha picha, Angela Tabiri
Mkulima mmoja alikuwa na aina tatu za wanyama.
Wote isipokuwa watatu ni kondoo, wote isipokuwa wanne ni mbuzi, na wote isipokuwa watano ni farasi. Sasa niambie, ana aina ngapi za kila mnyama?
Kama swali hili limekushangaza, basi hujakuwa peke yako. Jibu sahihi ni: kondoo watatu, mbuzi wawili, na farasi mmoja.
Kwa nini basi hisabati huonekana kuwa rahisi kwa baadhi ya watu na kuwa ngumu kwa wengine?
Ingawa vinasaba au sifa za kurithi zinaweza kuwa na mchango, hiyo ni sehemu tu ya fumbo kubwa linalohusisha muunganiko tata wa biolojia, saikolojia, na mazingira.
Utafiti kuhusu mwitikio wa watu kwa hisabati
Profesa Yulia Kovas, mwanasaikolojia na mtaalamu wa vinasaba kutoka Chuo Kikuu cha Goldsmiths, London, anachunguza kwa nini watu wana uwezo tofauti wa kihisabati.
Katika utafiti mkubwa, alifuatilia mapacha takribani 10,000 waliokuwa na uhusiano wa karibu au mbali wa kijeni, tangu kuzaliwa, ili kuchunguza jinsi vinasaba na mazingira vinavyoathiri uwezo wa kujifunza.
Anasema: “Utafiti wetu unaonyesha kuwa mapacha wanaofanana kijeni huwa na mfanano mkubwa zaidi katika kila sifa ya kisaikolojia kuliko wasiokuwa na ufanano huo.”
Hii ina maana kuwa pia wanafanana katika ujuzi wa hisabati, jambo linaloashiria kuwa mazingira ya familia siyo sababu pekee vinasaba vinaonekana kuwa na mchango mkubwa.
Kwa mujibu wa Profesa Kovas, vinasaba vinaweza kuchangia kati ya asilimia 50 hadi 60 ya uwezo wa watoto wa shule ya msingi katika hisabati.
“Ni wazi kuwa vinasaba na mazingira vyote vina mchango,” anasema.
Nafasi ya mazingira

Chanzo cha picha, djedzura/Getty Images
Mazingira tunayokutana nayo pia yana umuhimu mkubwa. Profesa Kovas anasisitiza kwamba siyo tu kuhusu kufanya vizuri shuleni au kusaidiwa kazi za nyumbani na familia inaweza kuwa jambo la bahati, kama kusikia kitu fulani redioni kinachoweza kubadilisha mwelekeo wa shauku au hamu yetu.
Aru Shinde, mwanafunzi wa shahada ya uzamivu (PhD) katika Idara ya Uhasibu, Chuo Kikuu cha Loughborough, anasema kwamba ingawa si kila mtu anaweza kuwa mhasibu, habari njema ni kuwa kila mtu anaweza kuboresha uwezo wake wa kihisabati.
Anasema kuwa ushahidi unaonyesha kuwa mawazo yetu, mitazamo, imani, na hisia vina mchango mkubwa katika kukuza ujuzi wa hesabu.
Hofu ya Hisabati
Aru anataja kuwa “hofu ya hisabati” inaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa utendaji wa mtu.
“Hofu hii husababisha mtu kuepuka masomo ya hisabati, hali ambayo hupelekea kushuka kwa ufaulu, jambo linaloongeza hofu zaidi.”
Wasiwasi huu huongeza mzigo kwenye sehemu ya kumbukumbu ya kazi, sehemu ya ubongo inayohusika na fikra na utatuzi wa matatizo.
Dr. Shinde anasema: “Wakati mtu ana wasiwasi, mawazo hasi huchukua sehemu kubwa ya kumbukumbu ya kazi, hivyo hakuna nafasi ya kutosha kwa mtu kuzingatia na kutatua tatizo.”
Anarejelea utafiti uliofanywa Chuo Kikuu cha Loughborough, uliowahusisha watoto wa miaka 9 hadi 10, ambao walifanya hesabu za akilini kwa tarakimu mbili, lakini walitakiwa pia kusikiliza na kurudia maneno fulani kabla ya kutatua swali.
Matokeo yalionyesha kuwa watoto waliokuwa na “hofu kubwa ya hisabati” walifanya vibaya zaidi, ikilinganishwa na wenzao.
Hisia asilia za nambari
Profesa Brian Butterworth wa Chuo Kikuu cha University College London, mtaalamu wa saikolojia ya utambuzi, anaeleza kuwa binadamu wana uwezo wa asili wa kuelewa nambari hata watoto ambao hawajafundishwa kuhesabu.
Hata hivyo, anaongeza kuwa kwa baadhi ya watu,
“Mfumo huu wa asili haufanyi kazi ipasavyo.”
Dyscalculia ni tatizo la kujifunza linaloathiri uwezo wa kuelewa na kutumia nambari na kiasi.
Profesa Butterworth anasema kuwa hali hii ni ya kawaida kama dyslexia, na huathiri takriban asilimia tano ya watu.
Watu wenye dyscalculia hupata ugumu kufanya hesabu rahisi kama tano jumlisha nane au sita jumlisha kumi na sita.
Butterworth na timu yake wameunda mchezo wa kielimu unaosaidia watoto, hasa wale wenye dyscalculia, kuelewa dhana za msingi za hisabati. Hata hivyo, bado haijathibitishwa iwapo msaada huo una athari ya muda mrefu.
“Unahitaji kuanza mapema na kisha kufuatilia maendeleo ya watoto hawa kwa miaka kadhaa,” anashauri.
Kujifunza hisabati ni kama kujenga ukuta
Dr. Shinde anafananisha kujifunza hisabati na kujenga ukuta wa matofali—ambapo msingi lazima uwe imara ili sehemu nyingine ziweze kujengwa juu yake.
“Huwezi kuacha matofali katikati. Kwa mfano, kama hukujifunza tukio fulani la kihistoria si tatizo kubwa, lakini kwenye calculus, hilo haliwezekani.”
Kujifunza kutoka kwa mataifa mengine
Profesa Kovas anarejelea Tathmini ya Kimataifa ya Wanafunzi (PISA) iliyoanzishwa mwanzoni mwa miaka ya 2000 kwa lengo la kupima ujuzi wa wanafunzi wa miaka 15 katika hisabati na sayansi, ili kulinganisha mifumo ya elimu duniani.
“Katika viwango vya kimataifa, wanafunzi kutoka China, baadhi ya nchi nyingine za Asia Mashariki, na Finland walikuwa miongoni mwa waliofanya vizuri zaidi.”
Je, tunaweza kujifunza kutoka kwa mataifa haya yanayoongoza?
Zhenzhen Miao, profesa msaidizi wa hisabati katika Chuo Kikuu cha Walimu cha Jiangxi, China, anasema kuwa hisabati nchini China inasisitiza:
“Maarifa ya msingi, ujuzi wa msingi, uzoefu wa msingi, na fikra za msingi za kihisabati.”

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Anasema kuwa nchini China, walimu na elimu vinaheshimiwa sana. Walimu hufundisha masomo moja au mawili tu, hivyo hupata muda wa kutosha wa maandalizi bora ya somo.
Pekka Räsänen, profesa wa sosholojia ya kiuchumi kutoka Chuo Kikuu cha Turku, Finland, anaeleza kuwa mfumo wa elimu nchini Finland pia unazingatia ujuzi wa msingi.
“Falsafa kuu ya elimu ya Finland ilikuwa kuhakikisha kila mwanafunzi anapata ujuzi wa msingi.”
Aidha, walimu nchini Finland hupata mafunzo ya kitaaluma kwa miaka mitano, na kwa kuwa taaluma ya ualimu inaheshimiwa sana, kuna waombaji mara kumi zaidi ya nafasi zilizopo.
Hata hivyo, Profesa Kovas anasisitiza kuwa tofauti zilizopo kati ya nchi hizo zinaonyesha:
“Ugumu na uhalisia wa changamoto hii ya elimu ya hisabati.”
Imetafsiriwa na Mariam mjahid