Wakili maarufu wa haki za binadamu, Peter Kibatala, ameiomba Mahakama Kuu kutoa amri ya dharura ili serikali ieleze alipo Humphrey Polepole, ambaye amedaiwa kutoweka katika mazingira yenye utata siku chache zilizopita.
Kibatala anasema hatua hiyo inalenga kuhakikisha haki na uwazi katika mwenendo wa mamlaka za usalama.
“Anapotoweka balozi ambaye amehudumia taifa katika nchi mbili, alikuwa msemaji au katibu muenezi wa chama cha mapindunzi, huyu mtu haiingii akilini, kimentiki, kisheria kwamba aanaweza kutoweka katika mazingira hayo aliyotoweka alafu mpaka leo hii tunazungumza hapa mahakamani hatuwezi kupata majibu”, alihoji Kibatala.
Kwa upande wa serikali, Wakili Mwandamizi Faraja Nguka ameiambia mahakama kuwa ombi la kumleta Polepole haraka “halitekelezekiā kwa sasa, akieleza kuwa kiapo cha Kibatala hakibainishi wazi ni nani anayemshikilia.
Nguka amesema ombi hilo linategemea mashaka zaidi kuliko ushahidi.
Hata hivyo, Kibatala amesisitiza kuwa wajibu maombi wote ni wawakilishi wa Jamhuri, hivyo wanapaswa kuhakikisha Polepole anafikishwa mahakamani.
“Ni njia nzuri ya uajibikaji”
Shauri hilo limevutia wanaharakati wa haki za binadamu na wanafamilia wa Polepole, wakiwemo mama yake AnaMaria Polepole na ndugu zake kadhaa waliokuwa mahakamani kufuatilia mwenendo wa kesi.
Miongoni mwa waliohudhuria pia ni Onesmo Ole Ngurumwa, Mkurugenzi Mtendaji wa THRDC, aliyesema hatua hiyo ni ishara muhimu ya kudai uwajibikaji wa vyombo vya dola.
“Ni njia nzuri ya uajibikaji, hasa pale unapokuwa na ushahidi kwamba vyombo vya serikali vinahusika.”
Mahakama imesema itatoa uamuzi wa maombi hayo saa nane mchana kwa saa za Afrika Mashariki.
Humphrey Polepole, ambaye kwa miezi ya karibuni amekuwa mkosoaji wa serikali ya chama tawala CCM, amewahi kushika nyadhifa kadhaa serikalini zikiwemo Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Mbunge, Mkuu wa Wilaya na Balozi wa Tanzania nchini Cuba, wadhifa aliouacha Julai mwaka huu.