Mvutano kati ya Eritrea na Ethiopia umechukua sura mpya baada ya serikali ya Eritrea kulaani shutuma za Ethiopia kuwa inajiandaa kuanzisha vita, ikizitaja kama “kauli za uchochezi wa kivita” katika eneo la Pembe ya Afrika linalozidi kukumbwa na hali ya sintofahamu ya kisiasa.

Kwa miezi kadhaa sasa, uhusiano kati ya mataifa hayo jirani umeendelea kuzorota, zaidi ya miongo mitatu tangu Eritrea ilipojitenga rasmi na Ethiopia mwaka 1993 baada ya mapambano ya silaha yaliyodumu kwa miaka kadhaa.

Barua yenye mashaka kwa Umoja wa Mataifa

Mapema mwezi huu, wizara ya mambo ya nje ya Ethiopia ilimwandikia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ikiishutumu Asmara kwa kushirikiana na kundi la upinzani Tigray People’s Liberation Front (TPLF) kuandaa vita dhidi ya serikali ya Addis Ababa.

Barua hiyo iliyotiwa saini na waziri wa mambo ya nje wa Ethiopia ilidai kwamba Eritrea na TPLF “zinatoa fedha, kuandaa na kuelekeza makundi yenye silaha” katika eneo la Amhara, ambako jeshi la serikali limekuwa likipambana na waasi kwa muda sasa.

Lakini Waziri wa Habari wa Eritrea, Yemane Ghebremeskel, amezipinga vikali tuhuma hizo, akisema Addis Ababa “inaendesha kampeni ya propaganda yenye malengo ya uchochezi na upotoshaji.”

“Kampeni hii ya kuchochea hisia za upanuzi wa mipaka imeambatana na kauli za vitisho na mbwembwe za kivita,” Ghebremeskel aliliambia shirika la habari la AFP, akiongeza kuwa barua ya Ethiopia kwa Umoja wa Mataifa ni “mchezo wa kisiasa wa udanganyifu.”

TPLF pia yajibu

Katika barua nyingine ya Jumatano iliyopokelewa na AFP siku ya Alhamisi, TPLF nayo imekanusha tuhuma hizo na kuziita “zisizo na msingi kabisa.”

Madonda yasiyopona kwa Wanawake wa Tigray

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Kundi hilo limesema lina wasiwasi kwamba serikali ya shirikisho “inaandaa mazingira ya vita vipya katika eneo hilo kwa kutumia madai yasiyo na ushahidi.”

“Hili ni jaribio hatari la kugeuza uhalisia – kumfanya mhalifu aonekane mhanga, na mhanga aonekane mhalifu,” ilisomeka sehemu ya barua hiyo iliyotumwa pia kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Historia ya uhasama

Baada ya Eritrea kujipatia uhuru mwaka 1993, vita vya mpakani vilizuka kati ya nchi hizo mwaka 1998 hadi 2000, na kusababisha vifo vya maelfu ya watu.

Uhusiano ulianza kuimarika mwaka 2018 baada ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed kusaini makubaliano ya amani na Rais wa Eritrea Isaias Afwerki, hatua iliyompatia Abiy Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2019.

Hata hivyo, uhusiano huo uliharibika tena baada ya Eritrea kuunga mkono jeshi la shirikisho la Ethiopia katika vita vya kaskazini mwa Tigray (2020–2022) ambavyo, kwa mujibu wa Umoja wa Afrika, viliua takribani watu 600,000.

Mvutano mpya kuhusu bandari ya Assab

Eritrea imepuuzilia mbali shutuma zilizotolewa na Ethiopia kwamba nchi hiyo inajiandaa kuanzisha vita ikisema ni ''matamshi ya uchochezi''
Eritrea imepuuzilia mbali shutuma zilizotolewa na Ethiopia kwamba nchi hiyo inajiandaa kuanzisha vita ikisema ni ”matamshi ya uchochezi”Picha: Getty Images/S. Gallup

Baada ya vita kumalizika, uhusiano wa mataifa hayo jirani umeendelea kuwa na baridi, huku Asmara ikiishutumu Addis Ababa kwa kuonesha tamaa ya kutaka kutumia bandari ya Assab iliyoko kusini mashariki mwa Eritrea.

Waziri Mkuu Abiy Ahmed amekuwa akisisitiza mara kadhaa kuwa Ethiopia — ambayo haina tena ufukwe wa bahari — inahitaji “ufikiaji wa bahari” kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi.

Kwa upande wake, Ghebremeskel ameishutumu Ethiopia kwa “kufufua ndoto za kiupanuzi” na kujaribu kudhoofisha uhuru wa Eritrea:

“Kwa miaka miwili sasa, sera ya Addis Ababa imejikita katika kutafuta njia za kupata ufukwe wa bahari — kwa njia za kisheria ikiwezekana, au kwa nguvu za kijeshi ikiwa italazimika,” alisema.

Mwezi Juni, ripoti ya kamati ya ufuatiliaji ya Marekani ilidai Eritrea inajenga upya jeshi lake na kuchangia hali ya kutokuwa na utulivu kwa majirani zake.

Lakini Eritrea ilijibu kwa hasira, ikisema ripoti hiyo “inapotosha ukweli” na kwamba Ethiopia ndiyo chanzo cha mvutano mpya katika eneo hilo.

Chanzo: AFP

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *