La Liga ya Uhispania na Serie A ya Italia zimepewa idhini kwa kusita na shirika la kandanda barani Ulaya UEFA kuandaa mechi moja kila moja nje ya nchi msimu huu, huku FIFA ikihitajika kutoa idhini ya mwisho kwa mpango huo.

Villarreal na Barcelona wanatarajiwa kucheza mjini Miami mwezi Desemba, huku AC Milan na Como wakipangwa kucheza mjini Perth, Australia mwezi Februari.

Mpango huo hata hivyo umekusolewa vikali na Rais wa Shirikisho la soka ulimwenguni FIFA Gianni Infantino.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Mkutano Mkuu wa Klabu za Soka za Ulaya (EFC) huko Roma, Infantino alisema: “Tuna muundo wa mashindano ambapo tunakuwa na mechi katika ngazi ya kitaifa, ya bara, na kisha ya kimataifa. Na huu ndio muundo ulioufanya mpira wa miguu kuwa mchezo namba moja duniani. Ikiwa tunataka kuvunja muundo huu, tunachukua hatari kubwa”, alisema Infantino. Kabla ya kuongeza :

“Ikiwa tunataka kuudhibiti, basi tunapaswa kuuchunguza kwa makini. Nina maoni yangu binafsi, ambayo sitawoshirikisha kwa sasa, lakini nimeona kuwa UEFA imeidhinisha mpango huo.”

“Je, tunataka kila mtu acheze kila mahali na afanye anachotaka?, alihoji Rais wa shirikisho la soka duniani FIFA.

Tunacheza kwa ajili ya mashabiki”

FC Barcelona yatwaa ubingwa wa ligi kwa ushindi katika pambano la jiji dhidi ya Espanyol
FC Barcelona yatwaa ubingwa wa ligi kwa ushindi katika pambano la jiji dhidi ya EspanyolPicha: Albert Gea/REUTERS

Mkurugenzi Mtendaji wa Bayern Munich, Jan-Christian Dreesen, alisema kuwa klabu yake haina nia ya kufuata nyayo za timu hizo nne zinazotarajiwa kucheza nje ya nchi. Dreesen, ambaye pia ni makamu mwenyekiti wa bodi ya utendaji ya shirikisho la vilabu vya soka vya Ulaya EFC, alisema:

“Nina mtazamo wazi kuhusu wapi pa kucheza mechi zetu za ligi tulizopewa wajibu wa kuzicheza, na ni nyumbani, kwa sababu tunacheza kwa ajili ya mashabiki. Tunacheza kwa mashabiki wa nje, lakini pia tunacheza kwa mashabiki wa nyumbani. Kwa hiyo, nafikiri ni wazo zuri kucheza mechi za ligi nyumbani na si nje ya nchi”, alisema Dreesen.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *