
Chanzo cha picha, Getty Images
-
- Author, Tom Bennett
- Nafasi, Jerusalem
Wapalestina katika Ukanda wa Gaza wamepata sababu ya kusherehekea kufuatia makubaliano ya kusitisha mapigano na mpango wa kuachiliwa kwa mateka.
Hata hivyo, wengi wao bado wanaogopa kukabiliana na huzuni kubwa iliyojengeka kutokana na vita vya miaka miwili.
“Asubuhi ya leo tuliposikia habari za makubaliano ya kusitisha mapigano, tulihisi furaha na maumivu kwa wakati mmoja,” alisema Umm Hassan, mwenye umri wa miaka 38, ambaye alipoteza mwanawe wa miaka 16 wakati wa vita, alipozungumza na BBC.
“Kwa furaha, vijana kwa wazee walianza kushangilia,” alieleza. “Lakini wale waliopoteza wapendwa wao walianza kuwakumbuka, wakijiuliza tutarudi vipi nyumbani bila wao.”
“Kila mtu aliyempoteza mpendwa anabeba huzuni hiyo kifuani, na anaona vigumu kufikiria kurudi nyumbani,” aliongeza.
Makubaliano hayo, yaliyotangazwa na Rais wa Marekani Donald Trump na ambayo tayari yameidhinishwa na Baraza la Usalama la Israel yanahusisha kuachiliwa kwa mateka hai 20 na miili ya mateka 28 waliokufa, kwa kubadilishana na wafungwa wa Kipalestina 250 waliofungwa kifungo cha maisha katika magereza ya Israel, pamoja na wafungwa wengine 1,700 kutoka Gaza.
Hii ni hatua ya kwanza ya mpango wa amani wenye vipengele 20, unaolenga kumaliza vita.
Hata hivyo, vipengele vilivyosalia bado havijajadiliwa.
“Sisi raia ndio tumebeba mzigo mkubwa wa mateso,” alisema Daniel Abu Tabeekh kutoka kambi ya wakimbizi ya Jabalia. “Makundi ya kisiasa hayaelewi maumivu yetu. Viongozi walioko nje ya nchi, wakikaa katika starehe, hawana hisia halisi za mateso tunayopitia hapa Gaza.”
“Sina nyumba,” aliongeza. “Nimekuwa nikiishi mitaani kwa mwaka mmoja na nusu.”Alisema haya alipokuwa akizungumza na BBC.
Israel ilianzisha mashambulizi Gaza kufuatia shambulio la Hamas la tarehe 7 Oktoba 2023, ambapo watu wapatao 1,200 wengi wao wakiwa raia wa Israeli waliuawa na wengine 251 kuchukuliwa mateka.
Kwa mujibu wa wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas, zaidi ya Wapalestina 67,000 wameuawa, wengi wao wakiwa raia.
Takwimu hizo zinatambulika kuwa za kuaminika na Umoja wa Mataifa na taasisi nyingine za kimataifa.
