Muhtasari
Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni, (WHO) linasema kuwa afya ya akili ni hali ya ustawi wa kiakili inayomwezesha mtu kukabiliana na misukosuko ya maisha, kufikia uwezo wake, kujifunza, kufanya kazi vizuri, na kuchangia katika jamii. Ni haki ya msingi ya binadamu na ina thamani ya binafsi na ya kijamii.
Afya akili ipo katika mwendelezo tata na inatofautiana kati ya mtu na mtu. Katika wakati wowote ule, sababu mbalimbali za mtu binafsi, familia, jamii na miundo ya kijamii zinaweza kuchangia kuimarisha au kudhoofisha afya ya akili. Ingawa watu wengi huwa na uwezo wa kustahimili matatizo, wale walioko katika mazingira magumu wana uwezekano mkubwa wa kupata hali za afya ya akili.

Mifano ya matatizo ya afya ya akili
Hali za afya ya akili ni pamoja na magonjwa ya akili, ulemavu wa kisaikolojia na hali nyingine zinazoambatana na msongo mkubwa, kushindwa kufanya kazi, au hatari ya kujiua. Magonjwa mengi ya akili yanaweza kutibiwa kwa gharama nafuu. Hata hivyo mifumo duni ya afya ina uwezo mdogo na kuna pengo kubwa la huduma duniani.
Vihatarishi vya afya ya akili
Sababu hizi hufanya kazi katika ngazi mbalimbali:
- Kibinafsi: Hisia, matumizi holela ya vilevi, vinasaba vinaweza kuongeza uwezekano wa matatizo ya afya ya akili.
- Kijamii na kimazingira: Umaskini, ukatili, ukosefu wa usawa, na mazingira duni huongeza hatari ya matatizo ya akili.
Visababishi hivi vinaweza kuanza katika hatua yoyote ya maisha, lakini vinapojitokeza wakati wa ukuaji wa awali, hasa utotoni, huwa na madhara makubwa. Malezi mabaya na adhabu za mwili huathiri afya ya akili ya watoto, na unyanyasaji wa watoto wakiwa shuleni pia ni sababu kubwa ya hatari.
Vigezo vinavyoweza kuzuia: Hivi navyo hutokea wakati wowote wa maisha na husaidia kujenga mnepo. Ni pamoja na stadi za kijamii na kihisia, mahusiano chanya, elimu bora, ajira yenye staha, ujirani salama na mshikamano wa kijamii.
Hakuna sababu moja inayoweza kutabiri kwa uhakika matokeo ya afya ya akili. Watu wengi waliokumbwa na hatari hawaathiriki vibaya, ilhali wengine huathiriwa vibaya bila sababu zinazoeleweka. Ni mwingiliano wa sababu hizi unaounda hali ya afya ya akili kwa muda mrefu.
Uendelezaji na uzuiaji wa magonjwa ya akili
Uendelezaji wa afya ya akili na uzuiaji wa matatizo ya akili hulenga kushughulikia sababu za mtu binafsi, kijamii na kimfumo. Mipango inaweza kulenga mtu binafsi, makundi maalum au jamii nzima.
Kwa sababu vichochezi vingi vya afya ya akili viko nje ya sekta ya afya, jitihada za uendelezaji na uzuiaji zinahitaji ushirikiano wa sekta mbalimbali kama elimu, ajira, sheria, usafiri, mazingira, makazi na ustawi wa jamii. Sekta ya afya inaweza kuchangia kwa kuingiza afua hizi katika huduma zake na kusaidia kuratibu jitihada za pamoja.
Kuzuia Kujiua
Kuzuia kujiua ni kipaumbele cha kimataifa na ni sehemu ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs). Mikakati muhimu ni:
- Kudhibiti upatikanaji wa njia za kujiua (kama vile sumu kali),
- Kukuza utoaji wa habari unaowajibika na sahihi kwenye vyombo vya habari,
- Kusaidia vijana barubaru kujifunza kukabili hisia
- Kutoa msaada wa mapema ili kuzuia kujiua.
- Kupiga marufuku matumizi ya viuatilifu vyenye sumu kali ni mojawapo ya mikakati ya bei nafuu na yenye ufanisi mkubwa wa kupunguza viwango vya kujiua.
Kuendeleza afya ya akili kwa Watoto na Vijana
Mbinu bora ni pamoja na:
- Sera na sheria zinazolinda afya ya akili,
- Msaada kwa walezi na wazazi,
- Mipango ya afya ya akili shuleni,
- Kuboresha mazingira ya jamii na mtandaoni.
Programu za kujifunza kijamii na kihisia katika shule zimeonekana kuwa na mafanikio kote duniani, hata katika nchi zenye kipato cha chini.
Afya ya akili pahala pa kazi
Hii ni eneo linalozidi kupewa kipaumbele. Inaweza kuimarishwa kupitia;
- Sheria na kanuni za kazi,
- Sera za kazini zenye mwelekeo wa afya ya akili,
- Mafunzo kwa wasimamizi,
- Afua maalum kwa wafanyakazi.

Mwanasaikolojia anasaidia familia kuondokana na kiwewe kilichotokea wakati wa mzozo wa kijeshi nchini Ukraine.
Huduma na matibabu ya afya ya akili
Mikakati ya kitaifa ya kuimarisha afya ya akili inapaswa kuzingatia:
- Kukuza ustawi wa wote,
- Kutoa huduma kwa watu wenye matatizo ya afya ya akili.
Huduma bora ni zile zinazotolewa katika jamii, ambazo ni rahisi kufikika, zinaheshimu haki za binadamu, na hutoa matokeo bora ya kupona.
Huduma hizi zinapaswa kujumuisha:
- Huduma za afya ya akili ndani ya vituo vya afya vya kawaida, kwa kushirikiana na watoa huduma wasio wa kitaalamu.
- Huduma maalum za kijamii, kama vile vituo vya afya ya akili vya jamii, timu za msaada wa kijamii, ukarabati wa kisaikolojia, msaada kutoka kwa watu waliopitia matatizo na makazi yenye msaada.
- Msaada wa afya ya akili katika maeneo yasiyo ya afya, kama huduma za ulinzi wa watoto, programu za afya shuleni, na magereza.
Kwa sababu ya pengo kubwa la huduma kwa hali kama msongo wa mawazo na wasiwasi, nchi zinapaswa kuzingatia njia bunifu kama;
- Matibabu ya kisaikolojia kutoka kwa wasio wataalamu,
- Zana za kidijitali za mtu kuweza kujihudumia mwenyeza, zana ambazo ni nafuu na zinaweza kufikia watu wengi kwa urahisi.
Hatua za WHO
Nchi zote wanachama wa WHO zimekubali kutekeleza Mpango Kabambe wa Afya ya Akili 2013–2030 unaolenga maeneo manne: Uongozi, Huduma za jamii, Uendelezaji na uzuiaji na takwimu.
Ramani ya mwaka 2024 inayoonesha hali ya Afya ya Akili duniani au Mental Health Atlas 2024 imeonesha kuwa hatua zilizopigwa ni chache na hazijafikia viwango vilivyokubaliwa.
Ili kuongeza kasi ya utekelezaji, ripoti ya WHO kuhusu afya ya akili inataja njia tatu;
- Kuthamini afya ya akili zaidi na kuwekeza kwa dhati kwa ushirikishwaji wa maana wa watu binafsi, jamii na serikali.
- Kubadilisha mazingira ya nyumbani, shule, kazi na jamii ili kulinda afya ya akili na kuzuia matatizo.
- Kuimarisha huduma za afya ya akili kwa kujenga mitandao ya huduma katika jamii ambazo ni nafuu, bora na zinakidhi mahitaji yote.
WHO inatilia mkazo: Haki za binadamu, kuwezesha watu waliopitia matatizo ya akili, kushiriki kikamilifu na kukuza ushirikiano wa sekta mbalimbali.
WHO inaendelea kushirikiana na mataifa kote duniani hata katika mazingira ya migogoro kutoa uongozi wa kimkakati, ushahidi, zana na msaada wa kiufundi kusaidia serikali na wadau kuleta mabadiliko ya pamoja kwa ajili ya afya bora ya akili kwa wote.