
Makubaliano yalifikiwa chini ya mpango wa amani ya Gaza wa Rais wa Marekani Donald Trump.
Mkutano huo unaotarajiwa kufanyika katika mji wa Sharm el-Sheikh, utaongozwa na rais Trump pamoja na rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sissi.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Misri Badr Abdel-Atti pamoja na mwenzake wa Marekani Marco Rubio walijadiliana kwa njia ya simu mipango ya mkutano huo lakini hadi sasa hakuna tarehe maalum iliyotolewa au taarifa zaidi juu yake.
Kinachojulikana ni kwamba viongozi wa kiarabu na wale wa Umoja wa Ulaya watashiriki mkutano huo.
Haya yanajiri wakati hii maelfu ya wapalestina waliokimbia makaazi yao wakirejea nyumbani baada ya Israel na Hamas kutia saini makubaliano hayo ya awamu ya kwanza ya usitishwaji mapigano Gaza.
Khalil Al-Deiri, ni mmoja wa wapalestina wanaorejea nyumbani.
“Tunatumai utakuwa usitishaji vita wenye baraka, wakati wa usalama na amani kwa watu wote. Tunatumai kwamba watu wote, raia wote wa mji wa Gaza, wataweza kurejea nyumbani.”
Msemaji wa ulinzi wa raia wa Gaza Mahmud Bassal amesema takriban wapalestina 200,000 wamerejea Kaskazini mwa Gaza.
Taarifa za hivi punde zinasema Hamas imesema suala la kuweka silaha zao chini kama moja ya masharti katika mpango wa Trump ni jambo lisiloweza kutekelezwa.