Afisa mkuu wa Hamas ameliambia shirika la habari la Agence France-Presse(AFP) siku ya Jumamosi kwamba zoezi la kuachiliwa kwa mateka 48, wengi wao wakiwa Waisraeli wanaoshikiliwa huko Gaza litaanza Jumatatu asubuhi. 

Imechapishwa:

Dakika 1 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

“Kwa mujibu wa makubaliano yaliyotiwa saini, ubadilishanaji wa wafungwa unatarajiwa kuanza Jumatatu asubuhi kama ilivyokubaliwa, na hakuna maendeleo mapya kuhusu suala hili,” Osama Hamdan amesema.

Baada ya hapo, Israel inatarajiwa kuwaachilia takriban wafungwa 2,000 wa Kipalestina kutoka katika magereza yake, kwa mujibu wa masharti ya hatua ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyopitishwa na Marekani yaliyotiwa saini na pande hizo mbili.

Wakati huo huo wajumbe wa Marekani Steve Witkoff na Jared Kushner wamehudhuria mkutano wa hadhara huko Tel Aviv siku ya Jumamosi ulioandaliwa na familia za mateka wanaoshikiliwa huko Gaza, kama makubaliano kati ya Israel na Hamas yanatoa fursa ya kuachiliwa kwao, kulingana na mwandishi wa shirika la habari la Agence France-Presse (AFP).

Steve Witkoff ametangaza, akihutubia moja kwa moja mateka wa Israel walioshikiliwa huko Gaza: “Mnarudi nyumbani.” Matamshi yake, yaliyotolewa katika “eneo la mateka,” yalipongezwa na kupigiwa makofi naa maelfu ya watu. Kisha, akihutubia familia za mateka, ameongeza: “Ujasiri wanu umewashangaza wengi duniani.”

Hamas inatazamiwa kuwaachilia mateka 48 – walio hai na waliokufa – kama sehemu ya makubaliano, ambayo usitishaji wa mapigano ulianza siku ya Ijumaa.

Iran inasema “haina imani” na Israel kuheshimu usitishaji vita

“Hakuna imani kabisa na utawala wa Kizayuni,” Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi amesema siku ya Jumamosi, akisema kwamba “kumekuwa na usitishaji mapigano mara kwa mara huko nyuma, katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Lebanon,” ambao “ulikiukwa” na Israel. “Tunaonya dhidi ya hila na usaliti wa utawala wa Kizayuni,” ameongeza kwenye televisheni ya taifa.

Hata hivyo, Bw. Araghchi amethibitisha tena uungaji mkono wa Iran kwa usitishaji mapigano Gaza siku ya Jumamosi. “Siku zote tumeunga mkono mpango au hatua yoyote ambayo inaweza kukomesha jinai hizi dhidi ya watu wa Gaza, kukomesha mauaji haya ya kimbari,” amebainisha waziri wa Iran.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *