Mapigano makali ya mpakani yamezuka kati ya majeshi ya Afghanistan na Pakistan huku vikosi vya nchi hizo mbili vikishambuliana kwa kutumia silaha nzito.

Mapigano hayo yalipamba moto jana Jumamosi siku moja baada ya serikali ya muda ya Afghanistan inayoongozwa na Taliban kulituhumu jeshi la Pakistan kuwa lilikiuka anga ya mji mkuu Kabul siku ya Alkhamisi usiku na kuripua soko moja kwenye eneo la Margha lililoko katika jimbo la Paktika linalopakana na Pakistan.

Islamabad haikuthibitisha wala kukanusha kuwa ilihusika na mashambulizi hayo lakini ilisema itatumia kila njia kuwalinda raia wake kwa sababu imekuwa ikishuhudia ongezeko la ugaidi inaouhusisha na kundi ililolipiga marufuku la Tehreek-i-Taliban Pakistan (TTP) ambalo inadai wapiganaji wake wanapewa hifadhi na serikali ya Taliban na kusaidiwa pia na hasimu wake India.

Hii ni katika hali ambayo serikali ya Kabul inasisitiza kuwa, haitaruhusu ardhi ya Afghanistan itumike dhidi ya nchi nyingine.

Duru za usalama za Pakistan zimevieleza vyombo vya habari kuwa, mapigano makali yamekuwa yakiendelea mpakani tangu jana jioni.

“Ufyatuaji risasi katika majimbo ya mpaka wa mashariki, ikiwa ni pamoja na Khost, Nangarhar, Paktika, Paktia, Kunar na Khost, unaendelea, na kuna ripoti za baadhi ya watu waliouawa au kujeruhiwa lakini hatuwezi kuthibitisha takwimu kwa sasa,” ameeleza afisa mmoja wa usalama wa Pakistan ambaye amevituhumu vikosi vya mpakani vya Afghanistan kuwa ndivyo vilivyoanza kufyatua risasi.

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Afghanistan, Enayatullah Khwarizmi, alitangaza usiku wa kuamkia leo kwamba vikosi vya Taliban vilifanya mashambulio ya “kujibu mapigo” dhidi ya wanajeshi wa Pakistan na kutoa jibu kwa “ukiukaji wa mara kwa mara” unaofanywa na nchi hiyo jirani dhidi ya mipaka ya Afghanistan na mashambulizi ya anga ndani ya ardhi ya nchi hiyo.

Mapigano hayo yameibua wasiwasi katika eneo na kupelekea nchi kadhaa ikiwa ni pamoja na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Qatar na Saudia Arabia kutoa miito kwa pande mbili kujizuia na kuonyesha uvumilivu…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *