
Mfuko wa Kuhudumia Watoto Umoja wa Mataifa wa (UNICEF) umetangaza kuwa, watoto 56,000 katika Ukanda wa Gaza wamebaki mayatima baada ya kupoteza mzazi mmoja au wote wawili katika kipindi cha miaka miwili ya vita vya jeshi la Israel katika uukanda huo.
Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) huko Palestina limeonya kuhusu hali mbaya ya watoto katika Ukanda wa Gaza na kusema: “Kwa mujibu wa takwimu, kwa akali watoto 56,000 wameachwa yatima wakati wa vita, na idadi hii inaongezeka kwa kutisha.”
UNICEF imesema katika ripoti yake ya hivi karibuni kwamba miaka miwili ya milipuko ya mabomu na vita imesababisha uharibifu mkubwa katika Ukanda wa Gaza, na kuua au kujeruhi zaidi ya watoto 64,000. Taarifa hiyo imeongeza kuwa watoto 320,000 walio chini ya umri wa miaka mitano katika Ukanda wa Gaza wako katika hatari ya utapiamlo na zaidi ya watoto 56,000 wamepoteza mzazi mmoja au wote wawili.
UNICEF imesema: “Tunakaribisha kwa mikono miwili usitishaji vita huko Gaza. Usitishaji huo wa vita unatoa matumaini kwa watoto ambao wameteseka na kutaabika katika miaka miwili ya vita vibaya.” Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa uliongeza: “Tuna zaidi ya malori 1,300 ambayo yako tayari kutuma na kusafirisha mahema, chakula, dawa na vifaa vya elimu hadi Ukanda wa Gaza.”
Ripoti ya UNICEF imetolewa huku usitishaji vita ukiwa umeanza kutekeleza katika Ukanda wa Gaza sambamba na kurejea maelfu ya wakazi wa Gaza waliolazimika kukimbia makazi yao.