Rais Andry Rajoelina atalihutubia taifa leo jioni baada ya maafisa waliojitokeza kuwaunga mkono vijana wanaoongoza maandamano nchini Madagascar, kutangaza kwamba wanashikilia udhibiti wa kikosi maalum cha jeshi la nchi hiyo.
Jana rais Andry Rajoelina alionya kuhusu jaribio la kufanyika mapinduzi ya kumpokonya madaraka wakati wanajeshi zaidi wakijiunga na maandamano ya vijana.
Shirika la habari la Reuters limetangaza leo Jumatatu, kwa kunukuu chanzo chake kwamba, maafisa wanaounga mkono maandamano ya vijana wakiongozwa na jenerali Nonos Mbina Mamelison wameshachukua udhibiti wa kikosi cha Gendermerie ambacho awali kilikuwa kikisaidiana na polisi kuwadhibiti waandamanaji.
Umoja wa Afrika umetoa wito wa utulivu na mazungumzo ili kuepusha taifa hilo la kisiwa kuingia kwenye machafuko zaidi.