Mateka

Jeshi la Israel linasema mateka wa kwanza wamekabidhiwa na Hamas na wamerejea Israel. Hadi Jumatatu, mateka 48 walikuwa bado wanazuiliwa huko Gaza, 20 kati yao wanaaminika kuwa hai.

Wote isipokuwa mmoja walikuwa miongoni mwa watu 251 waliotekwa nyara wakati wa shambulio la kundi la Wapalestina kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba 2023, ambapo takribani watu wengine 1,200 waliuawa.

Israel ilijibu kwa kuanzisha kampeni ya kijeshi huko Gaza, ambapo zaidi ya watu 67,000 wameuawa, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas.

Mateka ambao Israel inasema wameachiliwa

Israel ilishiriki picha za baadhi ya mateka walioachiwa huru wakikutana na IDF huko Gaza siku ya Jumatatu - pichani ni Ziv Berman

Chanzo cha picha, IDF

Eitan Mor, 25, alikuwa akifanya kazi kama mlinzi katika tamasha la muziki la Nova. Babake Mor alisema aliokoa makumi ya watu kabla ya kutekwa nyara na wapiganaji wa Hamas.

Mnamo Februari 2025, familia ya Eitan ilisema kuwa imepokea ishara ya uhai kutoka kwake. Miezi mitatu baadaye, walisema mateka aliyeachiliwa ambaye alitumia muda pamoja naye kwenye handaki alikuwa amewaambia jinsi alivyofanya kama “msemaji wa watekaji.”

Alon Ohel, 24, ana uraia wa Israel, Ujerumani na Serbia. Picha za Hamas zilionesha akichukuliwa mateka kutoka kwenye tamasha la Nova.

Alon hakuonekana kwenye video nyingine hadi Agosti 2025, aliporekodiwa akiendeshwa kuzunguka Jiji la Gaza akiwa na Guy Gilboa-Dalal.

Mwezi uliopita, familia ya Alon iliidhinisha kuchapishwa kwa video mpya ambayo walisema ilionesha alikuwa amepofuka jicho moja.

Gali na Ziv Berman, ndugu mapacha wenye umri wa miaka 28, walitekwa nyara kutoka Kibbutz Kfar Aza pamoja na jirani yao, Emily Damari.

Ziv alishikiliwa na Emily kwa siku 40 kabla ya kutengana. Aliachiliwa mnamo Januari 2025 wakati wa mpango wa kusitisha mapigano mara ya mwisho.

Familia ya Gali na Ziv ilisema walikuwa wamefahamishwa na mateka wengine walioachiliwa mapema 2025 kwamba bado walikuwa hai.

Mapacha Gali na Ziv Berman walichukuliwa mateka pamoja na jirani yao wa Uingereza na Israel Emily Damari, ambaye ameachiliwa huru.

Chanzo cha picha, The Hostages and Missing Families Forum

Guy Gilboa-Dalal, 24, alihudhuria tamasha hilo na kaka yake, Gal, ambaye alisema mara ya mwisho walipoonana ilikuwa ni kabla ya Hamas kuzindua msururu wa maroketi yake ya kwanza nchini Israel mwanzoni mwa shambulio hilo.

Gal aliwakwepa watu wenye silaha, lakini Guy alitekwa nyara. Mwezi uliopita, Hamas ilitoa video ikimuonesha Guy na mateka mwingine, Alon Ohel, wakiendeshwa kuzunguka Jiji la Gaza mwishoni mwa Agosti wakati jeshi la Israel likijiandaa kufanya mashambulizi huko.

Matan Angrest, mwanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) mwenye umri wa miaka 22, alikuwa kwenye kifaru kilichoshambuliwa karibu na uzio wa eneo la Gaza tarehe 7 Oktoba.

Video moja ilionesha umati wa watu ukimvuta kutoka kwenye tanki akiwa amepoteza fahamu na kujeruhiwa. Mapema mwaka huu, familia yake ilisema iliambiwa na mateka walioachiliwa kuwa alikuwa akisumbuliwa na pumu ya muda mrefu, kuungua bila kutibiwa na maambukizi.

Omri Miran, 48, alitekwa nyara kutoka nyumbani kwake huko Nahal Oz. Mkewe, Lishay, alisema alimwona mara ya mwisho akifukuzwa kwenye gari lake.

Yeye na binti zao wawili wadogo, Roni na Alma, hawakuchukuliwa pamoja naye. Mnamo Aprili 2025, Hamas ilitoa video ikimuonesha Omri akiadhimisha siku yake ya kuzaliwa ya 48. Kwa kujibu: Lishay alisema: “Siku zote nilisema na nilijua kila wakati, Omri ni mwokozi.”

Mateka ambao hali zao hazijulikani

Tamir Nimrodi, 20, alikuwa afisa elimu katika IDF katika Kivuko cha Erez mnamo 7 Oktoba. Mara ya mwisho mama yake, Herut, kumuona ilikuwa katika video ya kutekwa nyara kwake iliyowekwa kwenye mitandao ya kijamii siku hiyo.

Tangu wakati huo, hajapokea dalili za uwepo wa uhai wake na hatima yake haijulikani.

Bipin Joshi, 24, mwanafunzi wa kilimo wa Nepali, alitekwa nyara kutoka Kibbutz Alumim. Picha za tarehe 7 Oktoba 2023 zilimuonesha akitembea ndani ya hospitali ya al-Shifa katika Jiji la Gaza.

Familia yake haikupata dalili zozote za kuishi kwake kwa mwaka mmoja, hadi jeshi la Israel lilipotoa video ikimuonesha akiwa kifungoni Novemba 2023.

Familia hiyo ilitoa video hiyo kabla ya kutangazwa kwa usitishaji vita mpya, ikielezea kama “ushahidi wa uhai”. Hata hivyo, balozi wa Nepal nchini Israel sasa ameaimbia BBC kwamba mamlaka za Israel zimesema hakuna dalili zozote kwamba Joshi amenusurika.

Bipin Joshi

Chanzo cha picha, The Hostages and Missing Families Forum

Tamir Adar, 38, alikuwa mwanachama wa kikosi cha usalama cha jamii cha Nir Oz ambaye aliuawa wakati akipambana na wapiganaji wa Hamas wakati wa shambulio la Oktoba 7. Mwili wa mkulima huyo na baba wa watoto wawili unashikiliwa na Hamas huko Gaza.

Sonthaya Akrasri, 30, alikuwa mfanyakazi wa kilimo wa Thailand aliyeuawa katika shambulio la Kibbutz Be’eri, wizara ya mambo ya nje ya Thailand ilisema mnamo Mei 2024, ikitoa ushahidi uliopo. Mwili wake unashikiliwa na Hamas huko Gaza.

Muhammad al-Atarash, 39, alikuwa sajenti-mkuu katika IDF. Mnamo Juni 2024, IDF ilithibitisha kuwa baba wa watoto 13 kutoka kijiji cha Bedouin cha Sawa aliuawa wakati akipambana na wapiganaji wa Hamas karibu na Nahal Oz tarehe 7 Oktoba na kwamba mwili wake ulikuwa unazuiliwa Gaza.

Sahar Baruch, 24, alitekwa nyara kutoka Be’eri. Mnamo Januari 2024, IDF ilitangaza kwamba aliuawa wakati wa jaribio la uokoaji la vikosi vya Israeli huko Gaza. Haijabainika iwapo aliuawa na Hamas au milio ya risasi ya Israel.

Uriel Baruch, 35, alitekwa nyara kutoka kwenye tamasha la Nova. Mnamo Machi 2024, familia ya baba wa watoto wawili ilisema ilikuwa imefahamishwa na IDF kwamba aliuawa akiwa kifungoni huko Gaza.

Inbar Hayman, 27, alitekwa nyara wakati wa shambulio kwenye tamasha la Nova na aliuawa na Hamas akiwa kifungoni, familia yake ilisema. Yeye ndiye mateka wa mwisho wa kike kushikiliwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *