Huko nchini Tanzania, kumefanyika hafla ya maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Plan International Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Ofisi za Umoja wa Mataifa Tanzania, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), na lile linalojishughulisha na Masuala ya Wanawake (UN Women). 

Wimbi la matumaini likijidhihirisha katika nyuso za mabinti hawa, wanaoadhimisha siku yao muhimu – Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike, ambayo mwaka huu imebeba ujumbe unaosema, Mimi Mtoto wa Kike, Mimi Huongoza Mabadiliko: Wasichana Katika kitovu cha Migogoro

Kupitia programu yao ya kila mwaka ijulikanayo kama “Girls Take Over”, mabinti walipata fursa ya kuchukua nafasi za uongozi kwa siku moja katika taasisi mbalimbali — hatua inayolenga kuwapa uzoefu, ujasiri, na kuonesha uwezo wao katika kufanya maamuzi.

Miongoni mwao ni Hellen Natalis Kombe, aliyepata nafasi ya kuwa Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa kwa siku moja. Anasema kuwa uzoefu huo umemfundisha thamani ya uongozi na kufanya kazi kwa moyo.

Ningependa mashirika mengine yaweze kutoa nafasi kama hizi kwa watoto wa kike, — kwa sababu watoto wa kike wanaweza, na wana uwezo wa kufanya mambo mengi katika sehemu mbalimbali za uongozi, kwa sababu mtoto wakike ana sauti na anaweza.”

Magdalena Joseph naye ni miongoni mwa mabinti walioshiriki.

Anasema alipata nafasi ya kuwa Mkurugenzi wa Benki ya Stanbic Tanzania kwa siku moja, na uzoefu huo umemtia moyo zaidi.

Siku ya Kimataifa ya mtoto wa kike, inanikumbusha sana nafasi yangu, mimi kama bint, nafasi ya kuleta mabadiliko katika jamii, lakini pia kuwalinda mabinti wengine na kuwawezesha ili kufikia pale ambapo tunatamani kufika kama jamii.”

Maadhimisho haya yameacha alama ya matumaini kwamba mtoto wa kike anaweza kuongoza, kuamua, na kubadilisha dunia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *