
Huang ambaye mara ya mwisho kuhutubia Baraza ilikuwa mwezi Aprili mwaka huu, amesema katika miezi sita iliyopita, kumekuwepo na mafanikio kadhaa muhimu ya kidiplomasia ambayo yanaashiria mwanzo wa matumaini kwa amani ya kudumu.
Mathalani makubaliano ya Washington DC kati ya DRC na Rwanda, hatua iliyotajwa kuwa muhimu sana katika kupunguza uhasama na kuanzisha mchakato wa kuondoa vikundi vya waasi kama FDLR. Halikadhalika juhudi za Qatar zilizowezesha kutiwa saini kwa azimio la Kanuni za Majadiliano kati ya Serikali ya DRC na kundi la M23, pamoja na makubaliano ya kubadilishana wafungwa mapema Septemba.
Mikataba ya amani haiheshimiwi mashinani
Hata hivyo pamoja na hatua hizo, Huang amesema bado kuna wasiwasi mkubwa mashinani kutokana na kutozingatiwa kwa sitisho la mapigano.
“Makubaliano ya kusitisha vita hayajaheshimiwa. Pande zote zimeendelea kujiimarisha kijeshi na kurejea vitani. Mashambulizi yamesababisha ongezeko la wakimbizi wa ndani, ukiukwaji wa haki za binadamu na matatizo ya misaada ya kibinadamu,” amesema Huang.
Kutokana na kinachoendelea sasa amesema, “mapigano yanaelekea kusambaa hadi maeneo kama vile Kivu Kusini, jambo linalotishia kuzua vita vya ukanda mzima.”
Misuguano baina ya nchi jirani kuhusu mwelekeo
Changamoto nyingine aliyoiweka bayana ni kile alichoeleza kuwa ni kukosekana kwa muafaka miongoni mwa mataifa jirani kuhusu njia bora ya kuleta amani kunahatarisha mafanikio ya sasa.
Mapendekezo ya Huang
Huang amependekeza mikakati ifuatayo kama njia ya kuleta suluhu ya kweli:
- Sitisho la mapigano la haraka na bila masharti: Pande zote zinapaswa kutii maazimio ya Baraza la Usalama, ikiwemo Azimio 2773 (2025), na kuheshimu mikataba ya Doha na Washington.
- Utekelezaji wa mikataba iliyosainiwa: Utekelezaji wa makubaliano lazima upewe msaada wa kisiasa, kiufundi na kifedha.
- Umoja baina ya nchi za Afrika zinazosuluhisha: Ushirikiano kati ya Muungano wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa unapaswa kuimarishwa, kwa msaada wa viongozi wa kikanda.
- Kushughulikia chanzo cha mgogoro: Mikataba kama ile ya Addis Ababa inapaswa kufufuliwa ili kushughulikia matatizo ya kimuundo kama uporaji wa rasilimali.
- Ushiriki wa wanawake katika amani: Katika kuadhimisha miaka 25 ya Azimio la 1325, jitihada za kuwawezesha wanawake kushiriki katika mazungumzo ya amani zinaendelea kupewa msukumo.
Amani ianzie ndani ya moyo
Katika hitimisho la hotuba yake, Huang ambaye ametoa hotuba yake kwa lugha ya kifaransa, amesema “hakuna juhudi ya kimataifa itakayofaulu bila nia ya dhati kutoka kwa wahusika wakuu kwenye mzozo. Mataifa ya eneo hili lazima yaanzishe tena mazungumzo ya kweli na ya wazi ili kuhitimisha vita hivi mara moja na kwa wote.”