Taarifa iliyotolewa hii leo na ofisi ya haki za binadamu kutoka Geneva Uswisi na Addis Ababa Ethiopia imesema licha ya juhudi za zaidi ya miaka kumi kutoka Muungano wa Afrika na wadau wa kikanda kuunga mkono mchakato wa amani, viongozi wa Sudan Kusini wamesitisha kwa makusudi utekelezaji wa makubaliano ya amani, hali ambayo imerudisha taifa hilo ukingoni mwa vita kamili.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa mapigano yameripotiwa kwa kiwango ambacho hakijashuhudiwa tangu kusainiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano mwaka 2017, huku raia wakiendelea kubeba mzigo wa ukiukaji wa haki za binadamu na ukimbizi.

Kwa mujibu wa Tume, takribani watu 300,000 wameikimbia Sudan Kusini mwaka huu pekee kutokana na mapigano yanayoendelea. Wengine milioni mbili wamesalia wakiwa wakimbizi wa ndani, huku wanawake wakiathirika zaidi kutokana na vurugu na ukosefu wa usalama.

Tume hiyo imeitaka muungano wa Afrika kuharakisha kuanzishwa kwa Mahakama Mseto ya Sudan Kusini, kama ilivyoainishwa katika Sura ya Tano ya Makubaliano ya Amani ya mwaka 2018. Zaidi ya miaka kumi tangu kuzuka kwa vita mwaka 2013, waathiriwa bado hawajapata haki wala fidia.

Mwenyekiti wa Tume, Yasmin Sooka, amesema “Haki ni muhimu zaidi sasa kuliko wakati mwingine wowote. Ahadi zilizotolewa kwa waathiriwa lazima zitimizwe. Mahakama Mseto inapaswa kuanzishwa mara moja ili kuhakikisha uwajibikaji na kuimarisha utawala wa sheria.”

Wiki hii Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Baraza la Amani na Usalama la Muungano wa Afrika watakapokutana Addis Ababa na tume hiyo imeshauri mkutano huo kuweka haki na uwajibikaji kama kiini cha mijadala yao kuhusu Sudan Kusini, ikiwemo kuharakisha uanzishaji wa Mahakama Mseto.

Wasemavyo wajumbe wa Tume

Mjumbe wa Tume, Barney Afako, ameeleza mgogoro wa kisiasa unaoendelea, mapigano na rushwa ya mfumo mzima ni matokeo ya kushindwa kwa uongozi kutekeleza makubaliano ya mpito wa kisiasa. “Bila juhudi za dharura, za pamoja na endelevu za kidiplomasia, Sudan Kusini inaweza kutumbukia tena katika vita kamili vyenye madhara makubwa ya kibinadamu.”

Mjumbe mwingine wa Tume, Carlos Castresana Fernández, naye amesisitiza kuwa bila mifumo huru na ya kuaminika ya haki na uwajibikaji, nchi hiyo haitoweza kuvunja mzunguko wa ukatili na adhabu kwa wahalifu. “Umoja wa Afrika na washirika wa kikanda lazima wachukue hatua sasa siyo tu kuzuia vita vipya, bali kuweka msingi wa amani ya kudumu inayotegemea haki na utawala wa sheria.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *