Hisa ya sarafu ya Yuan ya China katika malipo ya biashara na upokeaji imefikia takriban 53%, na kuipita hisa ya dola ya 47%. Mabadiliko haya ya kihistoria yanakuja katika hali ambayo mwaka 2010 hisa ya Yuan katika biashara ya nje ya China takribani ilikuwa sifuri.
Takwimu za hivi punde zinaonyesha kuwa, Yuan ya China iliipiku sarafu ya dola katika biashara ya nje kwa mara ya kwanza mnamo 2023, na kuchukua hisa ya 53%, wakati hisa ya sarafu ya dola ikishuka hadi 47%.
Mabadiliko haya si tu ni mafanikio ya kiuchumi kwa China, bali pia yanaashiria mwanzo wa mpya katika mfumo wa fedha duniani; ukurasa mpya ambao dola si mchezaji pekee uwanjani na dunia inaelekea kwenye upande wa kukabiliana na sarafu ya dola.
Dola ya Marekani imekuwa sarafu kuu katika mfumo wa fedha wa kimataifa kwa miaka mingi. Ukiritimba huu umeipa kiburi Marekani cha kuweka vikwazo vya kifedha, kudhibiti mtiririko wa mtaji, na kuathiri sera za uchumi za mataifa ya dunia.
Hususan katika miongo ya hivi karibuni, hilo limeifanya Marekani mara nyingi kutumia vibaya dola kama chombo cha kutoa mashinikizo ya kisiasa na kiuchumi kwa mataifa mengine. Vikwazo vikubwa dhidi ya Russia, vikwazo vya kifedha dhidi ya Iran, na vitisho sawa na hivyo dhidi ya China yote hayo ni mifano ya Marekani kutumia sarafu ya dola kama wenzo na fimbo ya kuzichapia nchi nyingine hususan zinazokataa kudunishwa na kuburuzwa na serikali ya Washington.
Tabia na utendaji huu umezifanya nchi nyingi kufikia natija hii kwamba, kuwa tegemezi kwa sarafu ya dola ni hatari kubwa ya kimkakati kwa uchumi wao.
Katika radiamali kwa wasiwasi huu, nchi kama China, Russia, India, Iran na hata baadhi ya nchi za Ulaya zimeanza jitihada za kupunguza utegemezi kwa sarafu ya dola. Juhudi hizi zinapanuka katika mfumo wa kutumia sarafu za kitaifa katika biashara ya nchi mbili, kuunda mifumo ya malipo isiyotegemea SWIFT, na kupanuua njia za kubadilishana sarafu na washirika wa kibiashara.
Russia ikiwa moja ya mataifa yaliyokuwa mstari wa mbele katika njia hii, imetangaza kuwa, mauzo yake ya biashara na nchi za Asia ya Kati yamezidi dola bilioni 45, na sehemu kubwa ya mabadilishano haya ya kibiashara yamefanywa kwa kutumia sarafu za ndani. Rais Vladimir Putin wa Russia amesisitiza kuwa mwelekeo huu unapanuka kimfumo na unalenga kuongeza uhuru wa kifedha wa nchi hizo.

China pia imepiga hatua kubwa katika mwelekeo huu. Serikali ya Beijing imejaribu kutambulisha Yuan kama mbadala wa sarafu yu dola katika biashara ya kimataifa kupitia sera zenye uratibu na malengo.
Hatua hizi ni pamoja na kurahisisha udhibiti wa mtaji, kuongeza mvuto wa masoko ya fedha ya ndani kwa wawekezaji wa kigeni, kutolewa hati za kifedha za mikopo zenye thamani ya Yuan na nchi mbalimbali, na kuendeleza mfumo wa malipo wa CIPS kama njia mbadala ya SWIFT. Mradi wa sarafu ya kidijitali wa mBridge pia umezingatiwa kwa kutumia Yuan katika malipo ya kimataifa.
Kulingana na data za Benki ya Inayowezesha Miamala ya Kimataifa (BIS), kiasi cha biashara ya kimataifa ya Yuan kilifikia dola bilioni 817 kwa siku mwaka huu 2025, na kuongeza hisa yake ya jumla ya miamala ya fedha za kigeni hadi 8.5%. Ukuaji huu wa kuhisika umeifanya Yuan kuwa sarafu ya tano duniani ambayo inafanyiwa sana muamala na kuziba pengo na pauni ya Uingereza. Hii ni katika hali ambayo, hisa ya pauni katika biashara ya sarafu katika uga wa kimataifa imeshuka hadi asilimia 10.2, ikilinganishwa miaka mitatu iliyopita. Hivi sasa sarafu ya Yuan inakaribia kwa kasi nafasi ya nne duniani.
Lakini mabadiliko haya hayaishii tu katika takwimu na nambari. Kufuatia tangazo la Rais Donald Trump wa Marekani la kutoza ushuru wa asilimia 100 kwa bidhaa zote zinazoagizwa kutoka China, masoko ya fedha ya Marekani na kimataifa yalikabiliwa na hali ya kushuka kwa kuhisika.
Thamani ya soko la hisa la Marekani ilishuka kwa takriban dola bilioni 900, huku makampuni makubwa ya teknolojia kama Tesla, Amazon, Apple, na Nvidia yakipata hasara kubwa. Radiamali hii inasisitiza uwezekano wa uchumi wa dunia kuathiriwa na mivutano ya kibiashara na utegemezi mkubwa wa viwanda vya Marekani kwenye nyenzo na teknolojia ya China.
Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, kushadidi mivutano ya kibiashara kati ya Washington na Beijing, huku China ikifanikiwa kupanua nafasi ya Yuan katika biashara ya kimataifa, ni ishara ya mabadiliko makubwa katika mfumo wa uchumi wa kimataifa.
Ijapokuwa Trump aliweka ushuru kama hapo kabla na kisha akalegeza kamba, lakini hali ya sasa ya uchumi wa dunia, utegemezi mkubwa wa viwanda vya Marekani juu ya nyenzo na teknolojia ya China, na hali inayoongezeka ya kuielekea sarafu ya Yuan katika biashara ya kimataifa imepunguza uwezekano wa kurudi kwa urahisi katika hali ya awali.

Katika hali hii, nchi kama India, Brazil, Afrika Kusini, na hata baadhi ya nchi za Ulaya zinatafuta njia za kupunguza utegemezi wao kwa dola. Kundi la BRICS lina mipango ya kuunda sarafu ya pamoja au kuimarisha matumizi ya sarafu za kitaifa katika biashara zao za ndani. Hatua hizi zote zinalenga kujenga mfumo wa fedha wa pande nyingi na kukomesha satwa na ukiritimba wa sarafu ya dola.
Katika muktadha huu, utabiri wa Goldman Sachs unaonyesha kuwa, hali ya uchumi duniani inaingia katika awamu mpya; awamu ambayo Asia itakuwa mhimili mkuu wa ukuaji na maendeleo ya kimataifa.
Ingawa bado kuna safari ndefu kabla ya kupatikana sarafu mbadala wa dola, lakini treni ya kukabiliana na sarafu ya dola imeanza safari na inakata masafa kwa kasi. Katika njia hii nchi yoyote inayotaka kujinasua kutoka katika satwa ya kifedha ya Marekani haina budi kupanda treni hii. Kwa hakika, mustakabali wa uchumi wa dunia unategemea sarafu ambayo haijajengwa kwa kutumia nguvu na mabavu, bali kwa hali ya kuaminiana.