Rais wa Misri ameuambia mkutano wa kilele wa viongozi wa dunia siku ya Jumatatu kwamba pendekezo la Rais wa Marekani Donald Trump la Mashariki ya Kati ni “nafasi ya mwisho” ya amani katika eneo hilo na akasisitiza wito wake wa suluhisho la mataifa mawili, akisema Wapalestina wana haki ya kuwa na taifa huru.

Imechapishwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Mkutano huo wa kilele katika mji wa mapumziko wa Bahari Nyekundu nchini Misri wa Sharm el-Sheikh ulikuwa na lengo la kuunga mkono usitishaji vita uliofikiwa huko Gaza, kumaliza vita vya Israel na Hamas na kuendeleza maono ya muda mrefu ya kutawala na kujenga upya eneo lililoharibiwa la Palestina.

Mkutano huo ulionekana kuwa na lengo la kukusanya uungwaji mkono wa kimataifa kwa maono ya Trump ya kumaliza vita. Kiongozi wa Misri Abdel Fattah Al Sisi, mwenyekiti mwenza wa mkutano huo, amemwambia Trump kuwa “wewe tu” unaweza kuleta amani katika eneo hilo.

Mpango wa Trump unatazamia kuundwa kwa taifa la Palestina, lakini baada ya kipindi kirefu cha mpito huko Gaza na mchakato wa mageuzi unaoongozwa na Mamlaka ya Palestina inayotambuliwa kimataifa. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anapinga uhuru wa Palestina. Trump hakutaja suluhisho la serikali mbili katika mkutano huo.

Katika hotuba yake, Trump ametoa wito wa enzi mpya ya maelewano katika Mashariki ya Kati, akisema eneo hilo lina “fursa ya kipekee ya kumaliza mizozo ya zamani na chuki kubwa.” Amewataka viongozi “kutangaza kwamba mustakabali wetu hautatawaliwa na mapambano ya vizazi vilivyopita.”

Israel na Hamas zimekuwa chini ya shinikizo kutoka kwa Marekani, nchi za kiarabu na Uturuki kukubaliana juu ya awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa nchini Qatar kupitia wapatanishi. Mazungumzo yalianza siku ya Ijumaa.

Siku ya Jumatatu, Trump, Sisi, Amiri wa Qatar, na rais wa Uturuki wametia saini hati. Trump amesema hati hiyo inaweka “sheria na kanuni nyingi, na mambo mengine mengi, na ni ya kina sana.” Hati hiyo haikushirikiwa na waandishi wa habari au kuwekwa hadharani.

Mkutano huo ulifanyika muda mfupi baada ya Hamas kuwaachilia huru mateka 20 wa mwisho wa Israel walio hai na Israel kuanza kuwaachilia mamia ya Wapalestina kutoka magereza yake, hatua muhimu katika usitishaji mapigano. Hta hivyo, maswali muhimu yanabaki juu ya kile kinachofuata, na kuongeza hatari ya kurudi kwenye vita.

Zaidi ya viongozi 20 wa dunia walihudhuria mkutano huo akiwemo mfalme Abdullah wa Jordan, rais wa Ufaransa na waziri mkuu wa Uingereza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *