Rais wa Marekani Donald Trump amethibitisha kuwa atamkaribisha Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy katika Ikulu ya White House siku ya Ijumaa, wiki hii. Kauli hiyo imekuja muda mfupi baada ya Zelenskiy kutangaza kuwa anasafiri kuelekea Washington kwa mazungumzo muhimu kuhusu ulinzi wa anga na uwezo wa mashambulizi ya masafa marefu wa Ukraine.

Akizungumza akiwa njiani kurejea kutoka Mashariki ya Kati, Trump alisema, “Nadhani ndiyo, tutakuwa naye hapa Ijumaa,” akithibitisha ziara hiyo itakayolenga kujadili mustakabali wa msaada wa kijeshi wa Marekani kwa Ukraine. Mazungumzo hayo yanatarajiwa kujikita katika ombi la Kyiv la kupatiwa makombora ya Tomahawk, yenye uwezo wa kufika hadi Moscow — hatua ambayo Urusi imeitaja kuwa ni uchokozi mkubwa.

Marekani Washington D.C. 2025 | Mkutano kati ya Trump, Zelenskiy na viongozi wa Ulaya kuhusu mazungumzo ya Ukraine.
Trump na Zelenskiy wanatazamiwa kujadili uwezekano wa kuipatia Ukraine makombora ya masafa marefu ya Tomahawk.Picha: Alexander Drago/REUTERS

Ajenda ya mkutano kati ya Trump na Zelenskiy

Zelenskiy alisema tayari amempa Trump maelezo kuhusu idadi ya makombora wanayoyahitaji, akisisitiza kuwa mazungumzo ya kina yatafanyika ana kwa ana. Amesema anatarajia kujadili pia hatua za kuimarisha ulinzi wa anga wa Ukraine, hasa baada ya mashambulizi mapya ya Urusi kwenye jiji la Kharkiv, yaliyoharibu kituo cha afya na kukatiza umeme katika wilaya tatu.

Ziara hii inatarajiwa kuwa kipimo muhimu cha uhusiano kati ya Kyiv na Washington chini ya uongozi wa Trump, hasa katika kipindi hiki ambacho Marekani inachunguza kwa kina usawa wa msaada wake wa kijeshi kwa Ukraine na athari zake kwa usalama wa Ulaya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *