Makamu wa Rais wa Azam FC, Abdulkarim Mohamedamin Nurdin ‘Popat’ amethibitisha kwamba klabu yao imeanza kupokea mgao wa gharama za maandalizi kwenye mechi za hatua ya awali ya mashindano ya kimataifa, huku akibainisha kwamba fedha hizo zimekuwa na msaada mkubwa sana.
Popat amesema Azam ilianza kupokea kiasi cha Dola 50,000 (Sh122.1 milioni) za ushiriki wao wa mechi za hatua ya awali ambapo timu hiyo msimu uliopita ilishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.
Aidha Popat amesema, msimu huu ambapo Azam inashiriki Kombe la Shirikisho Afrika, wameshapokea kiasi cha Dola 100,000 (Sh244.3 milioni) za gharama hizo wakiwa wanakwenda kishiriki hatua ya pili ya mtoano.
“Azam tunaweza kuthibitisha haya anayoyasema Hersi, tulishapokea Dola 50,000 za msimu uliopita na tulizipokea muda mrefu tu,” amesema Popat.
“Msimu huu pia tumeshapokea kaisi cha Dola 100,000, kwetu ni daraja kwani zinakwenda kutusaidia kwenye gharama za uendeshaji wa timu kwenye mashindano haya ya Shirikisho.”

Popat amesema kufuatia usajili wa klabu kwenye umoja wa klabu Afrika (ACA) unaoongozwa na Mwenyekiti wake, injinia Hersi Said, Azam itakwenda kuwa moja ya klabu za kwanza kujiunga na umoja huo.
Kuanzia msimu uliopita klabu zinazoshiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika zimekuwa zikipewa fedha za maandalizi kiasi cha Dola 50,000, lakini msimu huu zimepanda na kufika Dola 100,000, huku ikitajwa hizo ni juhudi za Chama cha Klabu za Afrika (ACA) chini ya mwenyekiti wake, Hersi Said, kilichoanzishwa Novemba 30, 2023.