Paris, Ufaransa. Mama wa mchezaji supastaa, Mbappe amesema mwanaye huyo ambaye ni mchezaji wa Real Madrid “hana maisha” nje ya mchezo wa soka kwa sababu hapati muda wa kuanzisha uhusiano.
Staa huyo Mfaransa ni moja ya wachezaji wenye majina makubwa kwenye dunia ya mchezo wa soka hasa kutokana na kile anachofanya kwenye klabu yake ya Los Blancos.
Mbappe, 26, alifunga mabao 44 msimu uliopita baada ya kujiunga na Real Madrid akitokea Paris Saint-Germain na msimu huu ameshafunga mara 14 katika mechi 10.

Lakini, nje ya uwanja, Mbappe ameshindwa kabisa kuweka uwiano sawa wa maisha ya soka na maisha binafsi kwa maana ya vitu vya nje ya uwanjani kwa mujibu wa mama yake mzazi, Fayza Lamari.
Mwaka jana, ripoti kutoka Ufaransa zilifichua Mbappe anaweza kukabiliwa na tatizo la kiakili, kitu ambacho staa huyo baadaye alikikanusha. Lakini, mama yake, Fayza amesema anasikitishwa na hali ya maisha binafsi ya mwanaye, Mbappe.
Fayza amesema mwanaye hawezi hata kutembea mitaani hana hata muda wa kuwa na mpenzi.
Amesema: “Anasikia vizuri zaidi uwanjani kuliko nje ya uwanja. Hana maisha nje ya uwanja, lakini hayo ni maisha yake aliyochagua.
“Nilifanya naye mazungumzo mwaka jana wakati mambo yalipokuwa hayaendi vizuri. Nilimuuliza kama anataka mpenzi. Aliniuliza ‘Unamwona mwanamke kwenye hili tatizo?’ Hawezi hata kupita mitaani kuona kupoje. Inanihuzunisha sana.”
Mbappe huko nyuma aliwahi kuripotiwa kuwa na uhusiano na mrembo wa Kingereza, Georgia May na walionekana wakiwa pamoja kipindi cha likizo, Mei 2024.
Mrembo Georgia May kwa sasa ni mchumba wa aliyekuwa mchezaji mwenzake Mbappe huko PSG, kiungo Manuel Ugarte, ambaye kwa sasa anaichezea Manchester United.

Mama yake Mbappe, amesema alimwonya mwanawe kuwa hana muda anaweza kujikuta akipata tatizo la afya ya akili kama atashindwa kutafuta namna nzuri ya kuweka uwiano sawa wa mambo ya ndani ya uwanja na kuishi maisha mengine nje.
“Anaweza kupata tatizo la afya ya akili kwenye maisha yake. Ningependa kuzungumza naye juu ya hilo. Unaweza kuona mambo yalivyo. Hana maisha, hili linaweza kuwa tatizo kwake,” amesema.