Usemi wa ‘anayecheka mwisho ndio anacheka sana’ umetimia leo Jumanne, Oktoba 14, 2025 katika kundi C la mashindano ya kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026 kupitia Afrika.

Afrika Kusini ambayo kabla ya mechi za leo za kundi hilo ilikuwa nafasi ya pili kwenye msimamo, imejihakikishia tiketi ya Kombe la Dunia kwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 nyumbani dhidi ya Rwanda.

Na Benin ambayo ndio ilikuwa kinara wa kundi, imejikuta ikilia zaidi mwishoni kwani imeshindwa hata kumaliza katika nafasi ya pili kwenye kundi hilo ikianguka katika nafasi ya tatu baada ya kuchapwa mabao 4-0 ugenini na Nigeria.

Nchini Afrika Kusini kwenye Uwanja wa Mbombela, wenyeji maarufu kama Bafana Bafana wamemaliza mechi dhidi ya Rwanda kwa ushindi mnono wa mabao 3-0 uliowafanya wafikishe pointi 18 na kumaliza wakiwa vinara wa kundi.

Mashujaa walioifungia Afrika Kusini mabao ya kuivusha ni Thalente Mbatha, Oswin Appolis na Evidence Makgopa.

Furaha ya Afrika Kusini ilichagizwa zaidi na ushindi wa mabao 4-0 ambao Nigeria iliupata dhidi ya Benin ambayo ndio awali ilikuwa kinara wa Kundi C.

Aliyeibeba Nigeria leo ni Victor Osimhen ambaye amefunga mabao matatu huku bao lingine moja likipachikwa na Frank Onyeka.

Nigeria imemaliza katika nafasi ya pili katika msimamo wa kundi hilo ikiwa na pointi 17 na sasa ina uwezekano mkubwa wa kupata nafasi ya kucheza mchujo.

Kwingineko, ndoto za Uganda kucheza mchujo kwa kumaliza nafasi ya pili katika kundi G zilififishwa na kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Algeria.

Licha ya Steven Mukwala kuitanguliza Uganda kwa kuifungia bao katika dakika ya sita ya mchezo, Mohamed Amoura alifunga mabao mawili kwa mikwaju ya penalti katika dakika za 81 na majeruhi kuipa Algeria ushindi huo ulioifanya imalize ikiwa na pointi 24 kileleni mwa msimamo wa kundi hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *