
Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imepoteza mchezo wake wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Iran leo katika Uwanja wa Rashid, Dubai kwa mabao 2-0.
Mabao yote mawili ambayo Taifa Stars imeruhusu katika mchezo wa leo yamepatikana katika kipindi cha kwanza yakifungwa na Amirhossein Hossenzadeh na Mohammad Mohebi.
Hossenzadeh aliifungia bao la kwanza Iran katika dakika ya 17 kwa mkwaju wa penalti ambao timu yake iliupata baada ya Ibrahim Abdullah ‘Bacca’ kufanya faulo ndani ya eneo la hatari la Taifa Stars.
Dakika tisa baadaye, Mohebi aliiandikia Iran bao la pili akimalizia kwa shuti la wastani pasi ya Kasra Taher.
Matokeo hayo yalidumu hadi filimbi ya kumaliza mchexo huo ilipopulizwa.
Katika mechi ya leo, Taifa Stars ilifanya mabadiliko ya kuwatoa Israel Mwenda, Feisal Salum, Charles M’Mombwa, Paul Peter na Tarryn Allarakhia ambao nafasi zao zilichukuliwa na Abdul Suleiman, Morice Abraham, Lusajo Mwaikenda, Offen Chikola na Miano Van Den Bos.
Huo ni mchezo wa sita mfululizo kwa Taifa Stars kutopata ushindi tangu ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Madagascar kwenye mashindano ya CHAN 2024.
Baada ya hapo ilitoka sare tasa na Jamhuri ya Afrika ya Kati, ikafungwa bao 1-0 na Morocco, ikatoka sare ya bao 1-1 na Congo kisha ikapoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Niger na Zambia na leo imepoteza kwa Iran.