Straika, Alexander Isak ameonyesha hasira zaidi baada ya Sweden kushindwa kufanya vizuri kwenye mechi za kufuzu Kombe la Dunia licha ya kuwa na fowadi ya kiwango cha dunia.

Sweden ipo kwenye hatari ya kukosa fainali zijazo za Kombe la Dunia baada ya kuchapwa na Kosovo, Jumatatu ya Oktoba 13, 2025 huku kikosi chake kikiwa na washambuliaji wa maana kabisa.

Sweden sasa inashika nafasi za chini kwenye Kundi B ikiwa na pointi moja licha ya kikosi chake kuwa na mastraika Isak na Viktor Gyokeres, ambao walicheza kwa dakika zote dhidi ya Kosovo, ambayo ilikuwa imeshinda mara moja tu katika mechi 22 zilizopita.

Isak, ambaye alisajiliwa na Liverpool kwa ada ya Pauni 130 milioni kwenye dirisha lililopita, alikasirishwa na kitu hicho na kusema: “Sifahamu. Sisi wachezaji ni wa hovyo. Nilishasema hili, tunapaswa kuwajibika. Hebu tujitazame wenyewe kwenye vioo, hakuna ambaye ameonyesha tofauti. Si mchezaji mmoja mmoja wala si timu. Na bila shaka, kocha na watu wengine.”

SWE 01

Kocha Mkuu wa Sweden, Jon Dahl Tomasson yupo kwenye presha kutokana na matokeo ya timu hiyo kuwa ya hovyo na amesema: “Nina mkataba na Shirikisho la Sweden na tupo katikati ya mechi za kufuzu. Ni wazi hatupo vizuri na matokeo ni mabaya. Inaumiza kwamba tumesahau namna ya kufunga na sifahamu kwanini.”

Isak na Gyokeres wamekuwa kwenye wakati mgumu wa kufunga kwa sasa huko kwenye timu za zao za klabu Liverpool na Arsenal na hilo limeendelea kwenye timu yao ya taifa ya Sweden na kuiweka kwenye wakati mgumu wa kufuzu Kombe la Dunia 2026.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *