Kiungo wa Ivory Coast Pacome Zouzoua amekuwa staa wa kwanza kutoka Ligi Kuu Bara kukata tiketi ya kwenda kwenye Fainali za Kombe la Dunia akiwa kwenye kikosi cha Ivory Coast, baada ya nchi hiyo kuichapa Kenya 3-0.
Mabao ya Frank Kessie, Yan Diomande, Amad Diallo yametosha kuipa ushindi huo muhimu Ivory Coast iliyotawala mchezo kwa asilimia 63 na 37 kwa upande wa Kenya.

Ivory Coast ambao ni Mabingwa wa Afrika wamemaliza kinara kwenye kundi lao F ikifikisha pointi 26 baada ya kushinda mechi nane, wakitoa sare mbili ikiwa haijapoteza mchezo wowote, ikifuatiwa na Gabon wenye pointi 25, wakati Gambia ikimaliza ya tatu na alama 13.
Mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Alassane Outtara, Pacome ambaye ni staa wa Yanga aliingia dakika ya 61 akichukua nafasi ya Nicolas Pepe ikiwa ni mechi yake ya pili kucheza, baada ya kutangulia kucheza dakika 90 kwenye mchezo dhidi ya Shelisheli ambao Tembo hao walishinda kwa mabao 7-0.
Pacome anakuwa staa wa kwanza anayecheza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa Taifa lake kukata tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Marekani.
Staa mwingine wa Yanga Duke Abuya naye aliingia kipindi cha pili dakika ya 67 akichukua nafasi ya Michael Olunga kwenye mchezo huo.

Ivory Coast inaungana na Mataifa ya mengine nane ambayo yamefuzu moja kwa moja kwenye Kombe la Dunia 2026, yakiwemo Misri, Cape Verde, Tunisia, Morocco, Algeria, Ghana, Afrika Kusini na Senegal huku wakisubiri wengine wanaotokana na nafasi ya mshindani Bora.
Fainali za Kombe la Dunia 2026 zitafanyika kwa uaandaaji wa Mataifa matatu Marekani, Canada na Mexico zitakazoyahusisha majiji 16, zikitarajiwa kuanza Juni 11 hadi Julai 19, 2026.