
-
- Author, Asha Juma
- Nafasi, BBC Nairobi
Lucy Mocheche maarufu kama Mama Michael, ni mama ambaye leo anasimulia safari ya maisha ya mtoto wake wa kwanza.
Ukimuona Lucy akitembea njiani utadhani yuko sawa, lakini ukweli ni kwamba ana mengi mawazo yanayomzonga.
Alidhania malezi ya kifungua mimba wake yatakuwa rahisi lakini amekumbana na mitihani si haba ambayo imemuacha akibubujikwa na machozi usiku na mchana na kujiuliza maswali mengi bila kupata majibu.
Bi. Lucy alijifungua mtoto wake akiwa hajafikisha umri wa miaka 18, jambo ambalo lilimlazimisha kumuacha kijana wake alelewe na babu na bibi yake ili mwenyewe aweze kuendelea na masomo.
Bi. Lucy alimchukua mwanawe baada ya kuolewa na wakaanza kuishi kama familia, kipindi hicho kijana wake alikuwa katika hali nzuri.
“Michael alikuwa mtoto mwenye bidii sana, akiwa shule ya msingi, ile ya sekondari hadi kujiunga na chuo kikuu, mwanangu alinitii,” Lucy anasema.
Kijana wa Lucy alivyobadilika
Kijana wa Lucy, alifanikiwa kujiunga na chuo kikuu kimoja nchini Kenya. Shughuli zake aliziendesha kama kawaida, lakini alidai kuwa ili aweze kufanya vizuri zaidi katika masomo yake, aliomba atafutiwe nafasi katika shule ya bweni.
Lucy, alijitahidi kadiri ya uwezo wake kumtafutia mwanawe bweni kama moja ya mkakati wa kuendelea kufanya vizuri kimasomo, asijue kuwa huo ndio ulikuwa mwanzo wa kumpoteza mwanawe.
Ni lini hasa Michael alianza kubadilika? Mama Michael anakumbuka, “Mwaka wa pili ndio nilianza kuona mabadiliko akiwa tayari yuko kwenye bweni. Alikuwa anachukua muda mwingi kupokea simu. Kisha akawa anatoa sababu nyingi tu, mara alikuwa darasani, mara alikuwa na rafiki zake,” Lucy anasema.
Lucy anaongeza kuwa wakati huo ndio alianza kuona kuna shida, lakini hakujua kuwa itakuwa ya kumpotezea furaha hadi leo hii.
Lucy alivyoanza kuwa na mashaka na mwanawe

“Nilianza kuwa na mashaka na Michael wakati alikuwa anakaa tu akisoma masaa mengi. Na alikuwa akinywa sana kahawa. Kikombe kimoja kinakaa tu kwenye meza yake, chumbani kwake,” Mama Michael anasema.
Lakini wakati huo Lucy anasema hakufuatilia sana kutaka kujua anapikia wapi kahawa yake kwa sababu kulikuwa na jagi la kuchemsha maji.
“Huwa naskia aibu sana nikifikiria na kukumbuka ni wapi sikugutuka mapema kama mama. Mimi nilikuwa natoka, nikirejea nanunua kahawa fulani. Lakini nilijua mtoto wangu amepotea baada ya kugundua kahawa ambayo nimeweka mezani haipungui. Ila mwanangu anachemsha maji na kunywa kahawa kila wakati,” Lucy anasema.
Lucy anaongeza kuwa wakati alipojaribu kumuuliza kama hajafurahia kahawa ambayo huwa anamnunulia, Michael alikuwa mkali.
Kitu kingine ambacho pia mama huyu aligundua ni kuwa, upendo wa kijana wake kwa ndugu zake ulipungua.
Lakini dunia ina hulka moja, hakuna kinachoweza kuwa siri milele na pengine huenda siku ya ukweli kujulikana kwa Michael ilikuwa imefika.
“Mtoto wangu alipotea kwa siku mbili, sikumpata hata kwa simu. Siku ya tatu nikapigiwa simu ambayo iliniacha maisha yangu kwa mwanangu yakiwa yamebadilika kabisa,” Lucy anasema.
Lucy alipigiwa simu akiambiwa kuwa mtoto wake yuko hospitali na ikiwezekana afike mara moja. Alipofika, alimuona mtoto wake akiwa katika hali mbaya.
Madaktari wakamsihi asianze kumuuliza mambo mengi, badala yake amuache apumzike kiasi.
Lakini uchungu wa mwana aujuae ni mzazi, moja kwa moja, Lucy alipomtia machoni kijana wake, alianza kumuhoji ni wapi alipokuwa na nini kimetokea.
“Mama, nilitoka na wanafunzi wenzangu, tukaenda mahali wakanipatia spirit,” Michael alijibu bila kupinda.
‘Jinamizi la kahawa’ iliyompoteza mtoto wa Lucy

Baadaye sana ndio Lucy alikuja kugundua kahawa ambayo mwanawe alikuwa akinywa ilikuwa nini.
“Ghafla, uwezo wa mtoto wangu wa kuona ulipotea, hakutaka kunywa au kula kitu cha moto na ndani ya nyumba hakutaka kuona mwangaza,” Lucy anakumbuka.
“Hatimaye, nilikuja kugundua kuwa mwanangu anatumia dawa za kulevya, heroin na cocaine,” Lucy anasema.
Jambo jingine ambalo Lucy pia aligundua kwa mtoto wake, ni kwamba alianza kuwa msiri sana. Na hilo lilifanya iwe vigumu kujua alichokuwa anafanya.
Kilichosaidia kutambua kuwa Michael ni ametumbikia kwenye dimbwi la dawa za kulevya, ni wakati alipokuwa amelazwa hospitalini. Mama yake anasema alikuwa sawa na mtu ambaye amepoteza maisha. Hakujua aingiae wala atokaye.
“Hapo ndipo nilipata fursa ya kuenda kwenye nyumba ambayo mwanangu alikuwa anaishi. Na kukapatikana dawa nyingi za kulevya. Mwili wa Michael haukuwa unaitikia dawa yeyote. Hata adungwe au apewe dawa gani, hali yake iliendelea kuwa mbaya.
“Dawa zilizopatikana ndio zilisaidia madaktari kujua kile ambacho Michael alikuwa akitumia na hapo, ndipo walipojua nini cha kumtibu nacho kuokoa maisha yake,” Lucy anasema.
Lakini cha kushangaza kabisa ni kwamba, wakati mama Michael alikuwa ameenda kumuangalia kijana wake hospitalini kama ilivyokuwa kawaida baada ya mwanawe kuanza kupata afueni, alikutana na kitanda kitupu. Akiwa ameanza kufikiria pengine mtoto wake amepatwa na kitu kibaya, jibu alililopata hospitali lilimuacha kinywa wazi.
“Walisema alitolewa na watu ambao walijifanya kuwa ni jamaa wake na sikumpata tena mwanangu,” Lucy anasema.
Baada ya hapo walipoteleana kiasi cha haja hadi wakati fulani alipogundua kuwa kijana wake ameanza kupata matibabu katika kituo cha kurekebisha tabia, lakini cha ajabu, baada ya kusemekana kuwa hali ya Micheal imeimarika, alipewa ruhusa ya kutoka na hakuwahi kurejea nyumbani hadi hii leo.
Mwaka huu Micheal mwenyewe alianza kumtafuta mama yake kwa simu.
“Yeye akitaka kuzungumza na mimi ananipigia, lakini mimi nikitaka kuzungumza na yeye, siwezi kumpata kwa urahisi,” Lucy anasema
“Nilifika wakati nikahisi nimechoka sana moyo wangu, nikamuandikia ujumbe kumuarifu kuwa huenda ukawa ni wa mwisho maishani mwake, wakati huo nilikuwa nimelazwa hospitali na ndugu yake mdogo aliyehitaji kuongezwa damu. Hapo ndipo Michael alipokuja kutuona hospitali.
Kijana alifika hospitali na kumtolea mdogo wake damu.
“Mtoto wangu alifika hospitalini, lakini hakunijua na mimi sikumjua. Mara ya mwisho kuwa pamoja ilikuwa mwaka 2023 wakati anapewa matibabu katika kituo cha kurekebisha tabia, alikuwa amebadilika. Mtoto wangu alikuwa msafi, mzuri. Lakini wakati huu, Michael alikuwa amebadilika sana. Amezeeka. Alipofika karibu akacheka, ndio nilijua ni mtoto wangu,” Lucy anasema huku akidondokwa na machozi.
Kulingana na Lucy, kuna siku alimuona mtoto wake mahali kwa mbali, lakini hakuweza kumsongolea wala kuzungumza naye.
“Hiyo siku niliumia sana moyo wangu nikaanza kujiuliza, kwani hakuna mtu ambaye amemuona Michael, atake kujua yeye ametoka wapi, kwa nini yuko katika hali hii, ana wazazi au hana. Niliumia sasa,” Lucy anakumbuka.
Ushauri wa Lucy
Lucy anasema kile ambacho wakati mwingine hukaa akatamani, ni mtu ambaye anaweza kumfanya mtoto wake kwanza akajijua na kujimbua.
“Nataka mtoto wangu ajue kuwa yeye sio wa kwanza wala wa mwisho kujikuta katika hali kama hii. Watu wamkubali vile alivyo na arudi kusoma amalize masomo yake.
“Mzazi unaehangaika na mtoto wako, usichoke. Mtoto wako akiingia kwa uraibu wowote, usimkatae,” Lucy anashauri.