
Chanzo cha picha, MWANANCHI
Kuna tofauti nyingi kati ya nchi zilizoendelea na nchi masikini, lakini moja ya tofauti hizo ni ile inayohusu ajira au kazi. Kwenye nchi za dunia ya kwanza, kuna wingi wa ajira na uhaba wa watu. Na katika nchi za dunia ya tatu, kuna wingi wa watu na uhaba wa ajira.
Ripoti ya mwaka 2021 ya taasisi ya Twaweza inaonyesha matatizo makubwa yanayowaumiza Watanzania wengi, ni gharama kubwa za maisha, hii ilionekana kuwa kero kwa asilimia 56 ya wananchi, ukosefu wa ajira na fursa za kipato ulilalamikiwa na asilimia 50 huku asilimia 27 wakilalamikia uhaba wa chakula. Wengi walitaka serikali kushughulikia gharama za maisha, huduma za afya na huduma za usafiri.
Katika nchi masikini kama Tanzania, ajira ni tatizo kubwa kwa wengi, hasa vijana. Ni kadhia ambayo haiwezi kukosekana kwenye ripoti mbalimbali zinazoangazia maisha ya watu katika nchi za kipato cha chini.
Wakati huu Tanzania ikijiandaa na uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, na kampeni za wagombea mbalimbali zikiendelea. Swali linaloibuka: Je, ilani za vyama vya siasa zinazingatia mahitaji ya vijana?
Vyama na Vijana

Chanzo cha picha, CHAUMMA/CCM
Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu ameahidi kuweka mazingira wezeshi kwa vijana ili waweze kupata ajira. Ahadi hiyo ameitoa wiki kadhaa nyuma wakati akiomba ridhaa kwa wananchi mkoani Morogoro.
Mgombea huyo pia amenukuliwa na vyombo vya habari, akiahidi kufumua mfumo wa elimu ili kuhakikisha unaendana na wakati, ili kuwezesha wahitimu kushindana na soko la ajira. Kwa mujibu wa Mwalimu, amesema ataitisha mjadala wa kitaifa ili kujadili suala la elimu ndani ya siku 100 ya utawala wake kuangalia Tanzania inataka elimu ya namna gani ili kumuandaa mtoto.
Katika ilani ya chama cha Allience for Change and Transparency (ACT-Wazalendo) kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025. Moja ya vipaumbele vilivyoainishwa ni kujenga uchumi wa watu unaojitegemea na kuzalisha ajira milioni 12.
Ilani hiyo inasema, serikali ya chama hicho itatengeneza ajira mpya milioni 2.8 zitakazotokana na viwanda vinavyotumia malighafi za ndani kwa asilimia 85 katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake.
Kupitia ilani cha Chama cha Mapinduzi (CCM), katika uchaguzi huu, chama hicho kimeahidi kupunguza tatizo la uhaba wa ajira ikiwa kitaingia tena Ikulu, kwa kuajiri Walimu 7000. Pia itaajiri wahudumu wa afya wapya 5,000.
Ilani hiyo pia inasema, serikali ya CCM itatenga Bilioni 200 ili kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa Wafanyabishara wadogo. Jingine ni uanzishwaji wa programu maalumu za mitaa ya wiwanda Wilayani zenye kulenga kuzalisha ajira kwa Watanzania.
Ilani ya Chama cha Wakulima (AAFP) inasema chama kinakusudia kuzalisha ajira milioni 15 kupitia mfumo rasmi na mfumo usio rasmi na kuweka masharti nafuu kwa wawekezaji wazawa na wale wa kigeni. Kinaahidi kuweka mpango kwa vijana wote waliomaliza vyuo vya kati na vyuo vikuu katika ajira rasmi na zisizo rasmi kwa ajili ya uzalishaji mali.
NCCR-Mageuzi nacho kimeahidi neema kwa vija, ikiwa kitaingia Ikulu. Kinaahidi kuhamasisha vijana kuunda vikundi vya ujasiriamali ili kuweka mazingira bora ya kupata mikopo yenye riba nafuu na masharti nafuu.
Hakuna uhaba wa ahadi

Kwa hakika hakuna uhaba wa hadi za vyama vya siasa kwa vijana, hasa juu ya tatizo la uhaba wa ajira. Vyama takribani vyote vinaahidi na vinaendelea kuahidi mambo kedekede na mazuri.
Ingawa katika siasa, ahadi ya mwanasiasa ni jambo moja na utekelezwaji wa ahadi hiyo ni jambo jingine. Ahadi zote hizi si mpya, nyingi ya hizi husemwa kila uchaguzi unapokaribia. Tofauti tu kwamba CCM pekee ndio imepata nafasi ya kuzitekeleza kwa vitendo kwa vile ndio iko madarakani.
Je, utekelezaji walioufanya huko unatosha? Na kama umetosha kwa nini tatizo la ajira halifikii kikomo. Maswali haya yataendelea kubaki katika mjadala.
Nyingi ya ahadi hizi zinatekelezeka. Nchi ya Tanzania ina rasilimali nyingi ambazo zinaweza kusaidia wananchi kukwamuka ikiwa viongozi watazitumia ndivyo kwa manufaa ya raia.
Ajira ni mzizi wa kuondoa matatizo mengi – huduma binafsi ya afya ya mtu, huwa rahisi, chakula chake kinakuwa rahisi kukipata, uwezo wa kuhudumia familia unakuwa mwepesi. Kazi ni uti wa mgongo katika maendeleo ya jamii yoyote.
Katika nyakati hizi za msururu wa milipuko ya vijana wenye hasira katika mitaa na barabara za nchi mbali mbali, kutokana na sababu mbalimbali lakini ugumu wa maisha ukiwa chanzo kikuu, itakuwa dhambi na hatari kwa wanasiasa wanaotafuta nafasi ya kutumikia nchi, kulisahau kundi hili la watu.