
Rais wa Madagascar anayesakamwa na mashinikizo ya kujiuzulu, Andry Rajoelina ametangaza kulivunja Bunge kufuatia wiki kadhaa za maandamano dhidi ya serikali yake kote nchini, akisema ni muhimu kurejesha utulivu na kutoa nafasi kwa vijana.
“Nimeamua kulivunja Bunge la Kitaifa, kwa mujibu wa Katiba,” Rajoelina alisema hayo jana Jumanne kwenye mtandao wa kijamii wa X (Twitter).
“Chaguo hili ni muhimu ili kurejesha utulivu ndani ya taifa letu na kuimarisha demokrasia. Watu lazima wasikilizwe tena. Wape nafasi vijana,” ameeleza Rajoelina katika dikrii hiyo.
Hii ni katika hali ambayo, baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti kuwa Rais huyo wa Madagascar ameikimbia nchi hiyo na kuelekea Ufaransa. Vyombo vya habari vya Ufaransa vimeripoti kuwa Rajoelina alisafirishwa kutoka nchini kwake kwa ndege ya kijeshi ya Ufaransa.
Ripoti zinasema, Rais wa Madagascar alisema ameikimbia nchi kwa kuhofia maisha yake, kufuatia uasi wa kijeshi lakini hakutangaza kujiuzulu katika hotuba iliyotangazwa kwenye mitandao ya kijamii Jumatatu jioni akiwa katika eneo lisilojulikana.
Katika juhudi za kurejesha utulivu, Mkuu mpya wa Majeshi, Jenerali Demosthene Pikulas, amesema kuwa jeshi na gendarmerie linafanya kazi kwa ushirikiano kuhakikisha hali ya amani inarejea nchini.
Tangu Septemba 25, Rajoelina amekabiliwa na maandamano yanayoongozwa na vijana wa kizazi cha Gen-Z wanaolalamikia uhaba mkubwa wa maji na umeme, pamoja na madai ya rushwa; maandamano ambayo yameenea haraka kote nchini na kugeuka kuwa mashinikizo ya kumtaka ajiuzulu.