
MLANGO wa Gereza la Segerea lililopo, Tabata jijini Dar es Salaam ulifunguliwa na baada ya dakika chache, kikundi kidogo cha watu kilitoka.
Kikundi hiki kilikuwa cha baadhi ya waliokuwa wafungwa waliomaliza kutumikia adhabu zao.
Mmoja kati ya wafungwa waliotoka ndani ya gereza hilo alikuwa kijana wa kiume aliyekisiwa kuwa na umri uliokuwa unakaribia takribani miaka ishirini na tano.
Naye akiwa mmoja kati ya wafungwa waliokuwa wamemaliza vifungo vyao, aliruhusiwa kurudi uraiani baada ya kutumikia adhabu yake kutokana na makosa aliyokuwa ameyafanya.
Pamoja na kuachiwa huru, kijana huyu bado alionekana kutokuwa na furaha kama ilivyokuwa kwa wenzake wengine ambao alikuwa ameachiwa nao pamoja, walionekana kufurahi kurudishiwa uhuru wao wa kurejea tena uraiani.
Wakati wenzake wakichangamka na kushika njia kuelelekea vituoni baada ya kukamilisha taratibu zote, yeye bado alionekana kutawaliwa na unyonge na mawazo mengi kichwani mwake.
Ni kama mtu ambaye hakuwa akimini kama kweli alikuwa ameachiwa huru au alikuwa na kitu kingine kilichokuwa kinamtesa katika nafsi yake.
Ndiyo, kulikuwa na kitu kilichokuwa kikimtesa akilini mwake. Kitu kilichojificha ndani ya nafsi yake na kumfanya ashindwe kuufurahia uhuru wake.
Kitu gani kilikuwa kimimtesa? Labda alikuwa akiyafikiria maisha aliyokuwa akienda kuyaishi uraiani. Inawezekana pia, alikuwa akiujutia muda aliokuwa ameupoteza gerezani kwa kutumikia kifungo.
Au alikuwa akiyafikiria maisha aliyokuwa akiishi kabla ya kuhukumikiwa kifungo gerezani na wasiwasi wake ulikuwa kama angeweza kuyaishi tena maisha kama yale aliyokuwa akiishi kabla ya kukumbwa na hatia.
Wenzake walishafika mbali. Yeye akiwa bado katika hali ya unyonge alipiga hatua kuondoka katika eneo hilo lakini uso wake ulionyesha kutokuwa na furaha hata chembe.
Hata baada ya macho yake kuiona nuru mpya na pua yake kuvuta hewa safi iliyotoka kwenye miti iliyolizunguka eneo hilo la magereza, hakuonekana kuyafurahia mazingira hayo mapya.
Bado kichwa chake kilikuwa kimebeba mzigo mzito wa mawazo. Ni dhahiri maisha ya gerezani hayakumpendeza kutokana na kutokuzoea shida na vitendo vya kusumbuliwa kwa kupewa amri za kibabe kutoka kwa maaskari magereza na manyapara.
Haikuwa rahisi kuamini kama ni kumbukumbu mbaya za gerezani ndizo zilizokuwa zikimnyima furaha au kulikuwa na kitu kingine alichokuwa akikifikiria.
Ni nini kilikuwa kikimtesa…?
Mara baada kutoka nje ya gereza hilo, alishusha pumzi. Akaangaza macho yake kila pembe kama vile alikuwa mgeni asiyejua mwelekeo wake.
Bado hakuwa amepata utulivu wa akili, alifanikiwa kupiga hatua kadhaa kuondoka katika eneo hilo, lakini ghafla alisimama tena na kugeuka nyuma akalitazama lango kuu la gereza kisha akageuza macho yake kuuangalia muundo mzima wa jengo la gereza.
Laiti ungemuona ungeweza kudhani labda alikuwa ni msanifu majengo. Kwa dakika takribani tano, alivuta taswira iliyokuwa imejificha ndani ya jengo lililokuwa mbele yake.
Inaendelea…