
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Sayyid Abbas Araghchi amemkosoa vikali Donald Trump kwa sera yake ya kuchochea vita katika eneo la Asia Magharibi, akisema rais wa Marekani hawezi kudai anapigania kuleta amani katika eneo hilo huku akifuata sera za uchokozi na kufungamana na “wahalifu wa kivita.”
Katika andiko aliloweka kwenye mtandao wa X, Araghchi amesema madai ya hivi karibuni aliyotoa Trump kwamba Iran ilikuwa “wiki kadhaa” kutengeneza silaha za nyuklia kabla ya uvamizi wa Marekani na Israel dhidi ya vituo vyake vya nyuklia ni “uongo mkubwa.”
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha kuwa wenye maslahi ya kuuunga mkono utawala wa kizayuni wa Israel yako kazini kuilisha Washington taarifa za uongo za kiintelijensia.
“Ni wazi zaidi hivi sasa kwamba rais wa Marekani amekuwa akilishwa vizuri sana taarifa za uwongo kwamba mpango wa nyuklia wa amani wa Iran ulikuwa unakaribia kuunda silaha ifikapo msimu wa machipuo,” amesema Araghchi.
“Huo ni UONGO MKUBWA, na ilipaswa afahamishwe kwamba hakuna uthibitisho wowote wa hilo, kama ilivyothibitishwa na taasisi yake ya intelijensia.”
Araghchi amesema Trump aliingia madarakani na ahadi ya kukomesha “udanganyifu wa mfululizo inaofanya Israel kwa marais wa Marekani” na kukomesha ushiriki wa Marekani katika “Vita vya Milele” vilivyobuniwa na washupaliaji wa vita ambao kwa muda mrefu wamehujumu kufanya diplomasia na Iran.
Katika andiko lake hilo, mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran ameilaani Marekani kwa kuhusika moja kwa moja katika mashambulizi ya anga dhidi ya miji ya Iran mapema mwaka huu na kusababisha vifo vya zaidi ya raia 1,000 wakiwemo wanawake na watoto.
“Ni vigumu mtu kutambulika kama Rais wa Amani wakati anachochea VITA visivyoisha na kuungana na wahalifu wa VITA”, ameeleza Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran.
Araghchi amesema Trump “anaweza kuwa Rais wa Amani au Rais wa Vita, lakini hawezi kuwa wote wawili kwa wakati mmoja.”
Waziri wa Iran ameyasema hayo akiashiria jinsi Trump anavyojionyesha kuwa ni mpenda amani na matamshi yake kwamba “atajenga amani ya kudumu” katika eneo lote, huku akiwa kando ya waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.
Wakati huohuo, Araghchi amesema Iran ingali iko tayari kwa “mazungumzo ya kidiplomasia ya kuheshimiana na yenye manufaa kwa pande zote mbili,” lakini akasisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu haitavumilia vitisho au ulazimishwaji…/