Utawala wa kizayuni wa Israel umeueleza Umoja wa Mataifa kwamba utaruhusu malori 300 tu ya misaada kwa siku, ikiwa ni nusu ya idadi iliyokubaliwa kuingia katika Ukandwa Ghaza kuanzia leo Jumatano na kwamba hakuna mafuta yoyote au gesi itakayoruhusiwa kuingizwa katika eneo hilo isipokuwa kwa mahitaji maalumu yanayohusiana na miundombinu ya kibinadamu.

Hayo ni kwa mujibu wa waraka ambao shirika la habari Reuters limeuona na kuthibitishwa pia na Umoja wa Mataifa.

Olga Cherevko, msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu huko Ghaza, alithibitisha jana Jumanne kwamba umoja huo ulipokea barua kutoka kwa COGAT, kitengo cha jeshi la Israel ambacho “kinadhibiti mtiririko wa misaada” inayopelekwa Ghaza.

COGAT ilisema siku ya Ijumaa kwamba ilitarajia malori yapatayo 600 ya misaada kuingia Ghaza kila siku wakati wa usitishaji mapigano.

Hapo awali, Umoja wa Mataifa na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu zilitoa wito wa kufunguliwa njia zote za vivuko vya kuingilia Ghaza ili kuruhusu misaada inayohitajika sana katika ardhi hiyo ya Palestina iliyowekewa mzingiro.

Kwa mujibu wa taasisi hizo za kimataifa, makubaliano yanayolega lega ya ustishaji vita huko Ghaza, yaliyofikiwa chini ya mpango wa Rais wa Marekani Donald Trump, yanahitaji kuona njia zikifunguliwa ili misaada iweze kumiminwa kwenye eneo hilo linaloatilika kwa njaa.

Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kibinadamu OCHA Jens Laerke amesisitiza kwa kusema, “tunahitaji njia zote zifunguliwe.”

Laerke amebainisha kuwa Umoja wa Mataifa una tani 190,000 za misaada zinazosubiri na zikiwa tayari kupelekwa Ghaza…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *