Chama tawala cha Rais wa Gabon Brice Oligui Nguema, cha Muungano wa Kidemokrasia wa Wajenzi (Democratic Union of Builders) (UDB) kimepata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa Bunge, kwa kunyakua viti 102 kati ya 145 baada ya kutangazwa matokeo ya duru ya kwanza na ya pili ya uchaguzi wa wabunge uliofanyika nchini humo.

UDB ilishinda viti 50 katika duru ya pili ya upigaji kura uliofanyika siku ya Jumamosi, ikiwa imejinyakulia pia viti 52 katika duru ya kwanza iliyofanyika Septemba 27, na hivyo kupata asilimia 70 ya wawakilishi wa Bunge la Taifa. 

Hayo ni kwa mujibu wa matokeo yaliyochapishwa jana Jumanne na gazeti la kila siku la serikali L’Union.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, Chama cha Demokrasia cha Gabon, Gabon Democratic Party (PDG), kilichokuwa chama tawala lakini kinachomuunga mkono rais, kilipata viti 16 (vitano katika duru ya kwanza na 11 katika duru ya pili).

Nacho chama cha Rally for the Fatherland and Modernity (RPM) kilipata viti vitatu, huku National Union (UN) na Gabon Social Democrats (SDG) kila kimoja kikiambulia viti viwili.

Kila kimoja kati ya vyama vingine vidogo kilishinda kiti kimoja.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wabunge wengine saba walichaguliwa kama wagombea huru na viti vinne vimesalia kujazwa katika majimbo ambayo uchaguzi haukufanyika katika duru ya kwanza.

Matokeo rasmi yatatangazwa na tume ya uchaguzi mnamo siku zijazo.

Raia wapatao 900,000 wa Gabon walitimiza masharti ya kupiga kura katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa wabunge nchini humo, ambao ni wa kwanza tangu mapinduzi ya kijeshi ya 2023 yaliyomuondoa madarakani Rais wa zamani Ali Bongo.

Waangalizi wa kikanda kutoka Benin, Guinea, Mauritania na Togo walieleza katika taarifa ya pamoja siku ya Jumatatu kwamba duru ya pili ya upigaji kura ilifanyika katika hali ya utulivu licha ya kutokuwepo na msisimko.

Nguema alishinda uchaguzi wa rais wa Gabon Aprili mwaka huu…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *