.

Chanzo cha picha, Reuters

Aliyekuwa waziri mkuu nchini Kenya Raila Odinga amefariki akiwa na umri wa miaka 80.

Raila amefariki wakati akifanyiwa matibabu katika hospitali moja nchini India kulingana na duru za familia.

Odinga ambaye amemwacha mjane na watoto watatu ni mwanasiasa mashauhuri wa Kenya ambaye aliwahi kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo kuanzia 2008 hadi 2013.

Kabla ya kifo chake kiongozi huyo atakumbukwa kwa kupigania uhuru wa kidemokrasia, haki za kibinadamu na mabadiliko ya kitaifa.

Safari yake ya kisiasa

Raila Odinga alikuwa mtu mashuhuri katika siasa za Kenya na Afrika, na kutia moyo kizazi chote barani.

Akiwa mwana wa mpiganiaji uhuru Jaramogi Oginga Odinga, makamu wa kwanza wa rais wa Kenya, Raila alisomea Ujerumani Mashariki kabla ya kurejea nyumbani miaka ya sabini.

Aliwekwa kizuizini kwa miaka sita baada ya kutuhumiwa kuhusika na jaribio la mapinduzi mwaka 1982, na baadaye alikamatwa tena kwa kushinikiza demokrasia chini ya utawala wa chama kimoja.

Alirejea kutoka uhamishoni baada ya kuanzishwa tena kwa siasa za vyama vingi kabla ya kuchaguliwa kuwa Mbunge. Alikuwa na mchango mkubwa katika kukomesha utawala wa miongo kadhaa wa chama cha uhuru wa Kenya alipounga mkono jitihada za Mwai Kibaki za kuwania urais mwaka 2002.

Raila Odinga ambaye anajulikana sana kama Baba, aligombea urais mara tano, mara nyingi akiunganisha na kuunda upya upinzani, lakini hakuwahi kunyakua wadhifa huo wa juu zaidi.

Vita vyake vikali vilikuja kati ya mwaka 2007, wakati matokeo ya uchaguzi yaliogombaniwa kuzua ghasia nchi nzima, hatua iliosababisha makubaliano ya kugawana madaraka yaliyosimamiwa na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan.

Safari ndefu ya kisiasa ya Raila Odinga, iliyojaa ukakamavu, ukaidi na kujitolea mhanga, ilimletea sifa ndani na nje ya nchi.

Tunaendelea kukujuza…….

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *