Harakati ya Hamas imetoa tamko bila kutilia maanani mkutano wa kilele wa “Sharm al-Sheikh” ikisisitiza udharura wa kuzingatiwa haki halali za Wapalestina.

Katika taarifa hiyo, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu kwa ajili ya Ukombozi wa Palestina Hamas sambamba na kupongeza kuachiliwa huru wafungwa wa Kipalestina kutoka katika jela za kuogofya za utawala wa Kizayuni, imelichukulia suala hili kuwa mafanikio ya kihistoria ya kitaifa na kusema: ‘Muqawama na kuzingatiwa haki za taifa la Palestina ndiyo njia pekee ya kukomboa ardhi kutoka kwa utawala wa Kizayuni, kurejea wakimbizi na kuunda taifa huru la Palestina.’ Hamas imeonya kuwa viongozi wa utawala wa Kizayuni hususan Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu pamoja na Itamar Ben Gvir na Bezalel Smotrich, wajumbe wa baraza la mawaziri hawawezi kuwazuia wananchi wa Palestina kufurahia mafanikio ya muqawama wao.

Katika kikao cha Sharm el-Sheikh kilichofanyika nchini Misri Jumatatu, Oktoba 13, viongozi wa Marekani, walidai kuwa lengo kuu la kikao hicho lilikuwa ni kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano na kumaliza vita vya Gaza, huku harakati za muqawama wa Palestina kama vile Hamas na Islamic Jihad zikikataa kushiriki katika mkutano huo.

Muqawama wa Palestina unauchukulia mkutano wa kilele wa Sharm el-Sheikh kuwa usio halali wala usio na taathira yoyote katika kudhamini haki halisi za taifa la Palestina, na kwamba utaendelea kufuatilia vipaumbele vyake nje ya mwenendo wa diplomasia kwa kutilia maanani kwamba haukushirikishwa katika mkutano huo. Kutoaminika nafasi ya upatanishi ya Marekani, hasa ikitiliwa maanani kuwa imekuwa muungaji mkono mkuu wa kijeshi, kifedha na kisiasa kwa utawala wa Kizayuni, kumeufanya muqawama wa Palestina kuuona mkutano huo kuwa usio na maana katika utafutaji amani, bali ni maonyesho tu ya kisiasa.

Kikao cha karibuni cha Sharm Sheikh

Hossam Badran, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya Hamas ameonya kwamba iwapo usitishaji vita uliofikiwa utakiukwa na utawala wa Kizayuni, muqawama utajibu vikali ukiukaji huo na kwamba makubaliano ya aina yoyote hayapasi kuchukuliwa kuwa ni ulegezaji wa misimamo ya muqawama. Muqawama wa Palestina unaamini kwamba makubaliano yasiyo na dhamana ya utekelezaji wala kushirikishwa moja kwa moja pande zote husika hayawezi kudumu.

Muqawama wa Palestina unauchukulia mkutano wa Sharm el-Sheikh kuwa sehemu ya mchakato unaozingatia zaidi maslahi ya madola makubwa na ya utawala wa Kizayuni badala ya kuzingatia haki halisi za taifa la Palestina. Makundi ya muqawama wa Palestina yanasisitiza juu ya haki ya wakimbizi kurejea, kukomeshwa uvamizi, kusitishwa ujenzi wa vitongoji vya wolowezi wa Kizayuni na kuachiliwa huru wafungwa, na kuyapa kipaumbele masuala haya, hata kama hayatapewa uzito katika mazungumzo rasmi.

Serikali ya Marekani inadai kuwa ni mpatanishi katika hali ambayo ndiyo muungaji mkono mkuu wa kijeshi, kifedha na kisiasa wa utawala wa Kizayuni, na jambo hili limeufanya muqawama wa Palestina kuiona nafasi ya Washington katika mazungumzo hayo kuwa ya upendeleo na isiyo ya uadilifu. Muqawama wa Palestina hususan makundi ya Hamas na Jihad Islami, hauna imani na mikutano kama ya Sharm el-Sheikh kwa sababu unaichukulia mikutano hiyo kuwa sehemu ya michakato ya kisiasa ambayo badala ya kutambua haki za taifa la Palestina, hutumika zaidi kama chombo cha kuendeleza hali iliyopo ya kukaliwa kwa mabavu ardhi za Wapalestina na kudumisha maslahi ya utawala wa Kizayuni na madola ya Magharibi.

Hamas na Jihad Islami pia zinaichukulia mikutano ya kilele kama Sharm el-Sheikh kuwa batili, isiyo na matunda na inayokinzana wazi na matarajio ya taifa la Palestina, hivyo zinapendelea kufuatilia vipaumbele vyao kupitia uwanja wa mapambano na mazungumzo yasiyo rasmi na wapatanishi wa kieneo.

Maadamu mikutano kama ya Sharm el-Sheikh itaendelea kufanyika bila kushirikishwa pande kuu husika, bila kuzingatia haki za kimsingi za taifa la Palestina na kuendeshwa na madola ya Magharibi, bila shaka haitadhamini haki za Wapalestina. Hivyo Hamas na Jihad Islami zinauchukulia muqawama sio tu kama jibu kwa uchokozi unaofanywa na Wazayuni, bali pia kama mkakati wa muda mrefu wa kutambuliwa haki za taifa la Palestina. Makundi hayo yanaamini kuwa bila ya mashinikizo ya uwanjani na kudumishwa mapambano, hakuna utaratibu wowote wa kidiplomasia utakaoweza kukidhi matakwa ya Wapalestina.

Vyama vya Hamas na Jihad Islami

Mikutano ya kilele kama wa Sharm el-Sheikh, kwa mtazamo wa muqawama, inafanyika chini ya ushawishi wa Marekani na waitifaki wake wa nchi za Magharibi, ambao mara nyingi hutaka kudumisha hali iliyopo ya kukaliwa kwa mabavu ardhi za Wapalestina na kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni. Kutoaminika huku kwa nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani kunatokana na uzoefu wa kihistoria wa mikataba ya awali au usitishaji vita wa muda ambao uliuanzishwa kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni, huku haki halali za Wapalestina zikikanyagwa.

Kwa kutegemea uzoefu wa kihistoria, uchambuzi wa muundo wa kisiasa wa mikutano na kusisitiza misimamo ya muqawama, Hamas na Jihad Islami zimefikia natija kwamba haki za taifa la Palestina zinaweza kurejeshwa tu kupitia mapambano kwenye uwanja wa vita na mashinikizo ya kudumu, na kwamba mikutano ya kilele kama ya Sharm el-Sheikh haina nia yoyote ya kuwatendea haki Wapalestina, bali ni chombo tu kinachotumika kwa ajili ya  kudhibiti migogoro na kudumisha ukualiaji mabavu wa ardhi zao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *