
Marekani. Mwanamuziki na mwigizaji maarufu kutoka Marekani, Akon Thiam amekumbwa na sakata jipya katika ndoa yake, hii ni baada ya mkewe Tomeka Thiam kufungua kesi ya talaka huku akidai fidia ya Euro100 milioni.
Hata hivyo kesi hiyo imezua gumzo katika mitandao ya kijamii baada ya kugundulika kuwa mwanamuziki huyo ambaye amewahi kutamba na ngoma kama “Lonely” na “Smack That”, hana utajiri wowote. Kiasi cha pesa alichonacho ni dola 10,000, huku mali nyingine zikidaiwa kuandikishwa kwa jina la mama yake.
Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na tovuti mbalimbali za burudani mke wa Akon ameiambia mahakama ametaka fidia hiyo kutokana na ushiriki wake kwa miaka mingi katika mali za msanii huyo ikiwemo miradi ya muziki, makazi pamoja na biashara za nishati barani Afrika. Lakini wakati wa mchakato wa ukaguzi wa mali za Akon mahakama ilibaini kuwa akaunti ya Akon binafsi ilikuwa na kiasi kidogo sana cha fedha.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa mali zote zenye thamani kubwa zikiwemo nyumba, kampuni, na mapato ya muziki, zipo chini ya usimamizi wa mama yake na hivyo msanii huyo hana utajiri wowote anaomiliki yeye binafsi.
Utakumbuka mbali na sakata la Akon, staa mwengine ambaye alikumbana na sakata hilo ni beki wa timu ya taifa ya Morocco na klabu ya Paris Saint-Germain (PSG) Achraf Hakimi. Ambapo mwaka 2023, mke wake, Hiba Abouk, aliwasilisha ombi la talaka akitaka mgao wa nusu ya mali zake.
Hata hivyo, mahakama iligundua kuwa mali zote, ikiwemo nyumba, magari na akaunti za benki huyo, zilikuwa zimesajiliwa kwa jina la mama yake. Kwa mujibu wa taarifa, Hakimi alikuwa akipokea mishahara yake moja kwa moja kupitia akaunti ya mama yake, jambo lililomfanya aonekana hana mali binafsi kisheria huku mwanamitindo huyo ambaye alikuwa mkewe Hiba akiondoka kapa katika ndoa hiyo.