
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ametoa wito wa kuwepo umoja na mshikamano zaidi kati ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) ili kukabiliana na kuongezeka kwa misimamo ya upande mmoja na uvunjaji sheria unaofanywa na baadhi ya madola.
Sayyid Abbas Araqchi amesema hayo leo katika hotuba yake Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa unaofanyika mjini Kampala Uganda na kuelezea misimamo ya Iran katika masuala muhimu ya kimataifa.
Araqchi alisisitiza umuhimu wa kuzingatiwa kanuni za msingi za NAM, hususan haki ya mataifa kujitawala, kuheshimu kanuni na madhumuni ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa, kupiga marufuku matumizi ya nguvu na kulaani hatua za kulazimishana kwa upande mmoja.
Ametoa wito wa kuimarishwa mshikamano na umoja kati ya nchi zinazoendelea ili kukabiliana na changamoto zinazoongezeka na vitisho vinavyotokana na msimamo wa upande mmoja na ukiritimba baadhi ya mataifa makubwa.
Akigusia uvamizi wa kijinai uliotekelezwa na utawala wa Kizayuni na Marekani dhidi ya Iran mwezi Juni, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alilitaja hilo kuwa mfano wa wazi wa uvunjaji sheria.
Waziri wa wa Mashauuri ya Kigeni wa Iran pia alikariri tarehe ya kumalizika kwa muda wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo linahusiana na suala la nyuklia la Iran, mnamo Oktoba 18, akiwataka wanachama wa NAM kupinga matumizi yoyote mabaya ya taasisi za kimataifa – haswa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa – kwa kuchafua na kushinikiza mataifa yanayoendelea.