
Shinyanga. Serikali imeridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa kitaifa wa umeme jua unaotekelezwa katika wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga, ambapo hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 78.5.
Hayo yameelezwa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo ambao kukamilika kwake kutasaidia kufikia malengo ya ajenda ya kimataifa ya nishati endelevu kwa wote ifikapo mwaka 2030.
“Tumefika kujionea utekelezaji wa mradi huu na kiukweli nimeridhishwa na kasi ya utekelezaji ambayo mkandarasi amekuwa akienda nayo mpaka sasa, mradi huu ni sehemu ya jitihada za serikali kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma ya nishati safi, salama na nafuu, kukamilika kwake kutaongeza upatikanaji wa umeme vijijini na kupunguza utegemezi wa vyanzo vya nishati visivyo rafiki kwa mazingira,” amesema Mhandisi Mramba.
Kwa upande wake, Mhandisi msimamizi wa mradi huo Emmanuel Anderson amesema kasi ya ujenzi imeongezeka baada ya changamoto kadhaa zilizokuwa zikisababisha ucheleweshaji kutatuliwa na mkandarasi yuko katika hatua za mwisho za utekelezaji.
“Changamoto za awali kama ucheleweshaji wa vifaa na mvua nyingi sasa zimedhibitiwa, mkandarasi anaendelea kwa kasi nzuri na matarajio yetu ni kuona mradi unakamilika kwa muda uliopangwa” amesema Anderson.
Naye Meneja wa Kampuni ya Sinohydro inayotekeleza mradi huo, Daniel Xu amesema kampuni yake imejipanga kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa ubora unaohitajika na ndani ya muda uliowekwa,
“Tumeongeza nguvu kazi na vifaa kuhakikisha tunamaliza kazi hii kwa wakati, tunathamini ushirikiano mzuri tunaoupata kutoka serikalini na wananchi wa Kishapu tunaahidi kukamilisha mradi huu kwa viwango bora” amesema Xu.
Mhandisi huyo ameongeza kuwa, mradi huo unaotekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 325 chini ya utekelezaji wa kampuni ya Sinohydro kutoka nchini China, pia utazalisha Megawatt 150 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2025.
Hata hivyo kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kuongeza uwezo wa nchi katika kuzalisha umeme wa nishati jadidifu, kusaidia upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa taasisi, viwanda na wananchi, sambamba na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika mkoa wa Shinyanga na taifa kwa ujumla.