
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amegusia madhara ya mizozo, ugomvi, vita na uadui baina ya nchi za Kiislamu na kusema kuwa, hivyo ndivyo anavyotaka adui bali hayo ndiyo matokeo ya njama za maadui wa Uislamu na za Uzayuni wa kimataifa. Maadui wa Umma wa Kiislamu daima wamekuwa wakifanya njama za kuzusha mifarakano na kuzidhoofisha nchi za Kiislamu.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars, Rais Massoud Pezeshkian alisema hayo jana jioni na huku akiashiria mapigano yanayoendelea kati ya nchi mbili za Kiislamu za Afghanistan na Pakistan amesema kuwa, matukio ya kusikitisha yanayoendelea hivi sasa kati ya nchi hizo mbili ndugu za Kiislamu na jirani yamezusha wasiwasi mkubwa kwa nchi zote za eneo hili, ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Rais Pezeshkian vilevile amesisitiza kwa kusema: Nchi za Kiislamu, hasa mataifa yenye mizizi na tamaduni zinazofanana katika eneo hili, zina mshikamano usioweza kuvunjika wa imani, historia na utamaduni, na wote wanafungwa na amri ya Qur’ani Tukufu inayosema: “Hakika, waumini ni ndugu.” Hivyo mataifa hayo yana wajibu wa kufanya kazi pamoja kwani Waislamu wote wamo ndani ya chombo kimoja hivyo wanapaswa kudumisha amani, haki na maendeleo.
Vilevile amesema kuwa, matakwa ya Jamhuri ya Kiislamu ni kuhakikisha nchi za Kiislamu zinaishi pamoja kwa kupendana kwani mizozo na migogoro baina ya nchi za Kiislamu si matakwa ya mataifa yetu, bali ni matokeo ya njama za maadui wa Uislamu na za Uzayuni wa kimataifa.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia amesema kuwa, mazungumzo na kuimarisha uhusiano wa kidugu ndilo suluhisho la kupunguza mivutano baina ya nchi hizi mbili za Kiislamu na jirani yaani Afghanistan na Pakistan na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina imani thabiti na aya ya Qur’ani Tukufu inayosema: “Na shikamaneni na kamba ya Mwenyezi Mungu nyote, wala msifarikiane,” hivyo itatumia uwezo wake wote na kufanya juhudi zake zote kupunguza mivutano, kupanua utamaduni wa mazungumzo na kuimarisha uhusiano wa kirafiki kati ya nchi hizo mbili.