Kila kizazi kina wazo, ndoto na azma yake ya kuweka alama mpya katika ukuaji wa taifa. Miaka mingi iliyopita, Tanzania ilijikita katika Dira 2025, iliyokuwa mwongozo wetu katika kujenga msingi wa uchumi wa kati. Leo, tunapaa mbali zaidi na kuzindua Dira mpya ya 2050.

Lengo kuu la maono haya ni kuleta Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kati na juu, uliojaa fursa kwa wote, wenye kuendelea kimaendeleo na kijamii, na ambao unatumia rasilimali zake kwa ustahimilivu. Lakini safari hii ya kuweka alama mpya haitakiwi tu kuwa na mwelekeo wa kuelekea mbele; inatakiwa pia kutafuta ukweli na nguvu zilizomo ndani yetu wenyewe, katika chemichemi ya maarifa ya asili.

Maono ya kimataifa kama haya mara nyingi huwa na mwelekeo wa kutumia mifumo na teknolojia za kisasa za kigeni. Hilo ni jambo zuri na la lazima katika ulimwengu uliounganika. Hata hivyo, hatari ipo ya kupuuza na kuyafutilia mbali maarifa tuliyonayo kama Watanzania, yaliyokusanywa kwa nyongeza za vizazi vinavyopita.

Maarifa haya ni mkusanyiko wa ujuzi, mawazo, falsafa na mila chanya tulizorithi kutoka kwa mababu zetu. Yanajumuisha kila kitu, kuanzia mifumo ya kilimo inayolinda udongo na mazingara, hadi ujuzi wa matumizi ya dawa za asili kutokana na mimea ya misitu yetu; kutoka kwa hadithi na methali zinazokuza maadili ya ushirikiano na heshima, hadi ujuzi wa kitamaduni wa usimamizi wa misitu na maji.

Hizi sio tu “mambo ya zamani” zinazostahili kuepukwa. Ni mifumo thabiti ya ujuzi iliyothibitishwa na wakati na inayoweza kutoa suluhu za kipekee kwa chango zetu za kisasa.

Tukichunguza sekta ya kilimo, ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wetu, maarifa ya asili kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, aina za mbegu zinazostahimili ukame, na mbinu za kilimo cha asili zinaweza kuleta mchango mkubwa katika kuhakikisha chakula cha kutosha na usalama wa chakula.

Badala ya kutumia mbegu za kigeni na mbolea za kemikali pekee, kwa nini tusitumie maarifa yetu ya asili ya ukulima wa mseto na ulinzi wa mimea asili? Hii haitatuokoa tu gharama, bali pia itatulinda afya yetu na mazingara yetu.

Katika eneo la afya, asilimia kubwa ya Watanzania bado wanategemea matibabu ya asili. Ni muhimu kufanya tafiti ya mimea ya asili ambayo ni rasilimali ya kipekee ambayo inaweza kuundwa na kuleta dawa za bei nafuu kwa magonjwa mbalimbali. Kunaweza kuundwa jukwaa la kutatua utafiti wa kisayansi kwa ushirikiano na maarifa ya asili ya kimakabila na kuyafanya kuwa sehemu ya mfumo wetu wa afya.

Zaidi ya uchumi, maarifa ya asili ni nyenzo muhimu katika kulea dhana ya utanzania na uraia mwema. Hadithi, nyimbo, maigizo na sanaa zinafunza maadili ya ujumuishaji, heshima kwa wazee, upendo wa nchi na umoja. Elimu yetu ya msingi na ya juu inatakiwa kuwaunganisha maarifa haya ya asili katika mitaala, ili kizazi kijacho kikijue kuwa mafanikio hayamaanishi kuacha asili yao.

Hebu tusonge mbele kwa kutumia teknolojia ya kisasa, lakini tusisahau kuwa mababu zetu walituachia mwongozo ambao, kama tutauzungumza na kutumia, utatuongoza kwenye maendeleo ya kweli na ya kudumu. Ndoto ya 2050 iwe ndoto yetu sote, iliyojengwa juu ya ukweli wa Kitanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *