
Mwamko mkubwa wa Benki Kuu duniani kununua dhahabu kumeyafanya madini hayo kuwa ya pili miongoni mwa rasilimali kubwa zilizohifadhiwa hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya Benki Kuu ya Ulaya (ECB) iliyotolewa Juni mwaka huu. Hata hivyo, wachambuzi wanasema baadhi ya taasisi zinaonekana kuwa karibu kufikia kiwango cha kutosheka.
Kiwango cha dhahabu kinachomilikiwa na Benki Kuu sasa zimefikia viwango vilivyokuwa vimeonekana mara ya mwisho miaka ya 1960 tofauti na wakati huo hivi sasa bei yake imekuwa kubwa (Zaidi ya Dola 4,000 za Marekani kwa wakia moja).
Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa mwaka 2023, dhahabu na Euro zilikuwa karibu sawa, kila moja ikichangia takribani asilimia 16.5 ya akiba rasmi za fedha duniani kwa wastani. Mwaka 2024, uwiano huo uligeuka kuwa asilimia 16 kwa euro na asilimia 19 kwa dhahabu, huku dola ya Marekani ikibaki ikishikilia asilimia 47.
Kwa kawaida Benki Kuu hukusanya mali zenye ukwasi kama sarafu za kigeni na dhahabu kama njia ya kujilinda dhidi ya mfumuko wa bei na kueneza hatari katika uwekezaji wao. Pia huwapa uwezo wa kuuza akiba hizo ili kuimarisha sarafu zao katika nyakati za misukosuko.
Dhahabu huonekana kama chombo cha kuhifadhi thamani kwa muda mrefu na chenye uimara katika misukosuko, hivi sasa benki kuu zote duniani zinachangia asilimia 20 ya mahitaji ya dhahabu duniani ikiwa ni ongezeko kutoka asilimia 10 katika miaka ya 2010.
ECB ilibainisha kuwa utafiti wake unaonyesha dhahabu inazidi kuvutia nchi zinazoibukia na zinazoendelea ambazo zinahofia vikwazo (sanctions) na kupungua kwa nafasi ya sarafu kuu katika mfumo wa fedha wa kimataifa.
Kwa miaka ya hivi karibuni bei ya dhahabu imekuwa ikivunja rekodi za juu kila mwaka katika miaka ya karibuni. Hata hivyo mwaka huu imekuwa na mabadiliko makubwa sokoni kutokana na sera za ushuru za Marekani zinazobadilika haraka.
Mabadiliko makubwa katika soko la dhahabu yalitokea Februari 2022 wakati Urusi ilipoanzisha uvamizi wa moja kwa moja nchini Ukraine. Tukio hilo, liliambatana na mfumuko wa bei na matarajio ya kuongezeka kwa viwango vya riba, lilipelekea wawekezaji wengi kukimbilia kwenye mali salama kama dhahabu. Tangu wakati huo, hali ya sintofahamu ya kisiasa na kiuchumi imeendelea kuwa ya juu.
China imekuwa kinara wa kuongeza bei ya dhahabu, huku India na Uturuki zikiorodheshwa miongoni mwa wanunuzi wakubwa zaidi.
Dola yatetereka
Dola, ambayo kwa miongo kadhaa imekuwa sarafu kuu ya biashara na akiba ya kimataifa hivi sasa inakumbwa na changamoto kutoka kwa sarafu mbadala na mabadiliko ya kiuchumi duniani.
Mataifa mengi yanaanza kupunguza utegemezi wao kwa dola huku yakitafuta njia mbadala za kufanya biashara na kuhifadhi akiba zao. Hali hii inaleta maswali kuhusu mustakabali wa dola na athari zake kwa uchumi wa dunia.
Hali hiyo imeripotiwa katika vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa ikiwamo tovuti ya kimataifa ya biashara ya Wealth ambayo ilibainisha kushuka kwa thamani ya sarafu hiyo kwa asilimia 9.5 hadi kufikia Oktoba 8, 2025.
Tovuti hiyo inabainisha kuwa dola ya Marekani inashuka wakati ambao sarafu nyingine ikiwamo Euro ikiongezeka thamani kwa asilimia 12.6, Yuan ya China ikiongezeka kwa asilimia 2.6, Yen ya Japan (asilimia 6.4), Paundi (asilimia 7.3) Peso ya Mexico (asilimia 13.2).
Kwa mujibu wa Wealth mabadiliko ya sera za kiuchumi na mtiririko wa mitaji vinaweza kuathiri sarafu kwa njia tofauti kwa wakati mmoja.
Hilo linaripotiwa na Wealth ikiwa ni miezi michache tangu kituo cha Habari cha Aljazeera kuripoti kushuka kwa thamani ya Dola kwa asilimia 10.8 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2025.
Jambo hili ambalo halijawahi kutokea tangu mwaka 1973 linachangiwa na sera za kiuchumi za Rais Donald Trump zinazowachochea wawekezaji wa kimataifa kuuza akiba zao za dola jambo linalotishia hadhi ya dola kama “sarafu salama” ya kuhifadhi thamani na uchumi wa nchi.
Nini maana yake?
Mtaalamu wa Uchumi na Biashara, Oscar Mkude amesema kushuka kwa thamani ya dola kunafanya bidhaa zinazotoka Marekani kuwa nafuu na inaweza kuwa na habari njema kwa wanunuzi waliopo sehemu tofauti duniani.
Pia hali hiyo itafanya bidhaa za Marekani kushindwa kushindana vizuri kwenye masoko makubwa kama yale ya umoja wa Ulaya ambayo yanatumia sarafu tofauti.
“Utapata bidhaa kwa gharama nafuu ni ahueni upande mmoja lakini ni habari inayoumiza kwa watu wanaouza bidhaa za Marekani na wale wanaoiuzia Marekani,” amesema.
Hali hiyo itafanya sasa sarafu shindani kuendelea kuwa imara na kushika masoko ya kimataifa japokuwa anasema suala hilo halitabiriki kuwa litadumu kwa muda gani.
Amesema jambo hilo linaweza kuwa limeathiriwa na vitu vingi ikiwamo sera za tozo zilizowekwa na Marekani jambo ambalo linachochea hata wabia wa kibiashara kuanza kitafuta njia mbadala za kuwekeza katika masoko mengine.
“Wanakosa imani kwa kuona kama Rais huyu ameweka vikwazo hivi akija mwingine anaweza kuweka vingine zaidi. Watu wanaanza kutafuta namna nyingine ya kuwekeza katika maeneo mengine yatakayowapa uhuru wa biashara bila kuwa na athari hasi,” amesema.
Amesema siku chache zijazo Marekani pia itatangaza kushuka kwa riba, jambo ambalo litafanya waliowekeza katika Dola ya Marekani mapato yao kushuka.
“Sera hizi za kiuchumi zinaweza kuwa moja ya sababu ya kushuka kwa Dola ya Marekani dhidi ya fedha nyingine zenye nguvu,
Kwa wale wauzaji wa bidhaa kama Tanzania inayouza kahawa nayo inaweza kujikuta inapata fedha ndogo japokuwa upande wa pili itakuwa ni ahueni ya kutumia fedha ndogo katika kununua bidhaa kutoka nje ya nchi.
“Matokeo yake watumiaji wa bidhaa kama mafuta wataona bei inapungua jambo litakaloleta ahueni. Bidhaa za utalii wanaolipwa kwa Dola na kutapata kiasi kidogo cha fedha japokuwa kwa upande wa shilingi ya Tanzania haitaathiriwa sana kwa sababu bado iko imara,” amesema.
Mtaalamu wa uchumi na Biashara, Dk Donath Olomi amesema dola ikishuka ina pande mbili, ambapo upande mmoja ni wa faida na mwingine ni hasara.
Kwa waagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi watapata bidhaa kwa bei rahisi kama ikiwamo malighafi jambo ambalo linapunguza gharama na kuwafanya waweze kushindana sokoni.
“Kwa walaji hata mafuta tunaona yanashuka ni faida kwetu. Lakini kama unazalisha kwa ajili ya kuuza nje utapata fedha kidogo. Kwa ujumla kitu kizuri kwenye kubadilishana fedha ni uthabiti, dola ikiwa inapanda sana inakuwa si jambo zuri inafanya watu washindwe kufanya miradi kwa uhakika pia ikiwa inapanda na kushuka ni tatizo ikikaa katika eneo moja ni nzuri,” amesema Dk Olomi.
Akieleza namna ambayo wafanyabiashara wanaweza kukabiliana na kushuka kwa thamani ya dola ya Marekani sokoni amesema upo uwezekano wa wao kuangalia eneo lingine japokuwa itahitaji muda mrefu kuwa na uhakika.
“Kiuhalisia huwezi kubadilisha mwelekeo kwa haraka sana kwa sababu mahusiano ya biashara ya kimataifa yanakuwa ya muda mrefu. Unaweza kubadilisha uelekeo kwenda katika soko lingine hadi unafika huko unakuta thamani ya fedha unayoitaka imepungua tayari na kule ulipokimbia thamani imeongezeka,” amesema.
Pia amesema hiyo inaweza isiwe rahisi kwa sababu biashara nyingi zinafanyika kwa mikataba ya muda mrefu huku akitolea mfano wa wachuuzi wa kahawa kuwa huenda wameshanunua bidhaa za mwaka.
Ni neema kwa Tanzania
Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, anasema kuongezeka kwa mahitaji ya dhahabu duniani kumeleta athari chanya katika uimara na thamani ya Shilingi ya Tanzania.
Tutuba anasema kiasi cha dhahabu kinachouzwa nje kimeongezeka kwa kiwango kikubwa. Kwa mara ya kwanza, bei ya dhahabu imefikia Dola 4,063 kwa wakia moja, ikichochewa na ongezeko la mahitaji ya wawekezaji katika kipindi cha sintofahamu ya kiuchumi duniani.
“Kuongezeka kwa mauzo ya dhahabu nje ya nchi kunasaidia kuongeza upatikanaji wa dola nchini Tanzania. Benki Kuu ya Tanzania inanunua dhahabu moja kwa moja kutoka kwa wachimbaji, ambao ama huuza kwa benki kuu au kuiuza nje, hivyo kusaidia kuongeza fedha za kigeni katika uchumi,” alisema Gavana Tutuba.
Alisema mahitaji ya bidhaa za kuagiza kutoka nje yamepungua kutokana na kuimarika kwa viwanda vya ndani vinavyozalisha bidhaa kama vigae, vioo na samani, hivyo kupunguza utegemezi wa bidhaa za kigeni.
Tutuba pia anaeleza athari chanya za sheria mpya inayowataka wananchi kufanya miamala yote ya ndani kwa kutumia shilingi ya Tanzania badala ya dola za Marekani.
“Sera hii imesaidia kuimarisha shilingi kwa sababu bidhaa na huduma za ndani sasa zinalipiwa kwa sarafu ya taifa, huku dola zikitumika tu katika biashara za nje,” anafafanua.
Mbali na dhahabu, sekta nyingine zimechangia katika kuimarika kwa sarafu. Sekta ya utalii, hasa Zanzibar na Arusha, imepata nafuu kubwa baada ya kuporomoka kutokana na janga la Uviko-19, huku mauzo ya mazao ya kilimo kama mahindi, maharage, mchele na karanga yakiendelea vizuri.
“Mauzo makubwa ya dhahabu, kupungua kwa uagizaji bidhaa kutoka nje, usimamizi makini wa sarafu, sheria zenye kuunga mkono uchumi na ongezeko la mauzo yasiyo ya jadi, yote yamechangia kuimarika kwa thamani ya shilingi ya Tanzania,” anasema Gavana Tutuba.