
Gavana wa Sinai Kaskazini nchini Misri amesema mamia ya malori ya misaada yapo tayari kuingia katika Ukanda wa Gaza kupitia kivuko cha Rafah, lakini yanasubiri kibali cha utawala wa Israel ili yaingize misaada hiyo ya dharura.
Utawala haramu wa Israel ulifunga kivuko cha Rafah na kuzuia misaada ya kibinadamu kuingia Gaza siku ya Jumatatu, kutokana na mzozo na Hamas kuhusu kurejeshwa kwa miili ya mateka.
“Hatuko tayari kwa 100% tu, lakini 1,000% tayari kwa hali yoyote ijayo au maagizo yoyote yaliyotolewa na jimbo la [Misri] kuhusu kuingia kwa msaada wa kibinadamu au kupokea waliojeruhiwa na waliojeruhiwa,” amesema Khaled Megawer, Gavana wa jimbo la Sinai Kaskazini la Misri, ambalo linapakana na Gaza.
Duru za habari zinaarifu kuwa, baadhi ya malori ya misaada ya kibinadamu yalianza kuingia Gaza kupitia vivuko vingine jana Jumatano.
Siku ya Jumanne, Israel ilitishia kupunguza kwa asilimia 50 kiwango cha misaada ya kibinadamu inayoruhusiwa kupelekwa Gaza, chini ya makubaliano tete ya kusitisha mapigano na Hamas.
Wakati huo huo, Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Tom Fletcher, ameitaka Israel kufungua mara moja vivuko zaidi katika Ukanda wa Gaza ili kuruhusu ongezeko la utoaji wa misaada.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Jumatano, Fletcher amesema kuwa Umoja wa Mataifa unatafuta msukumo mkubwa wa misaada ya kibinadamu kwa Gaza, akisisitiza kuwa, mamia ya malori ya misaada yaliyoidhinishwa kuingia katika eneo hilo la Palestina ni machache, kwani maelfu yanahitajika kwa ajili kupunguza janga la kibinadamu katika eneo hilo.