Aliyekuwa Mkurugenzi wa michezo wa AS Roma ya Italia, Ramón Rodríguez Monchi, amefichua jinsi alivyoweza kuongeza kwa kiasi kikubwa ada ya uhamisho ya Mohamed Salah, aliyetimkia Liverpool mwaka 2017.

AS Roma ilikuwa inammiliki nyota huyo kutoka Misri, baada ya kumsajili moja kwa moja kutoka Chelsea mwaka 2016, ambapo kabla ya hapo Salah aliichezea klabu hiyo ya mjini Roma kwa mkopo.

Mochi amesema baada ya kupokea ofa ya Liverpool, kama kiongozi wa juu alijifungia na kuchezesha bei ya kuuzwa kwa Salah, ambaye alionekana kuhitajika kwa namna yoyote ile na majogoo hao wa jijini Liverpool.

MO 01

Kiongozi huyo mstaafu amesema Liverpool ilimuhitaji Salah kwa ada ya euro 33 milioni, lakini kwa utashi wake binafsi aliiongeza ada hiyo na kufikia euro 55 milioni, ambazo zililipwa ili kukamilisha mpango wa uhamisho wa mchezaji huyo.

Monchi aliajiriwa AS Roma na kuwa mkurugenzi wa michezo wa Roma, Aprili 2017 baada ya mafanikio makubwa akiwa Sevilla. Hata hivyo, alipojiunga na klabu hiyo ya mji mkuu wa Italia, uhamisho wa Salah ulikuwa tayari unaendelea. 

Miezi miwili baada ya Monchi kuwasili ndani ya klabu hiyo ya Stadio Olimpico, Salah akaondoka.

Akizungumzia hali ya uhamisho huo, Monchi alieleza kuwa alipoingia Roma, tayari mazungumzo ya kumuuza Salah kwenda Liverpool yalikuwa yamefikia hatua ya mwisho. 

Amesema mchezaji huyo alikuwa tayari ameonyesha nia ya kuondoka, na klabu zote mbili zilikuwa zimefikia makubaliano kuhusu ada ya uhamisho. Hata hivyo, Monchi alihisi kuwa AS Roma ilipaswa kudai fedha zaidi kwa mchezaji wa kiwango kama cha Salah.

MO 02

“Ilikuwa ni lazima. Nilipowasili, Salah alikuwa karibu kuuzwa kwa euro 33 milioni pamoja na bonasi ya milioni tatu. Mwishowe, aliuzwa kwa euro 55 milioni, lakini tayari kulikuwa na makubaliano na mchezaji. Alitaka kuondoka, na kitu pekee tulichoweza kufanya ni kushinikiza kupata dau kubwa zaidi.

“Lazima uelewe kipindi hicho. Uuzaji wa Salah ulikuwa kabla ya Dembele, kabla ya mlipuko wa soko la usajili na ada kubwa kupita kiasi. Na, nasisitiza, tayari kulikuwa na makubaliano kati ya AS Roma na Liverpool. Kile tulichofanya ni kusukuma tu tupate kadri ya uwezo wetu, kwa sababu mchezaji tayari alijua anataka kuondoka,” amesema.

Salah alicheza msimu mmoja akiwa AS Roma, baada ya kujiunga na klabu hiyo kutoka Chelsea mwaka 2016. Hata hivyo, uhamisho wake kwenda Liverpool ulikuwa wa mafanikio makubwa, kwani ameweka historia kubwa katika klabu hiyo na kujithibitisha kuwa mmoja wa wachezaji bora kabisa katika historia ya Ligi Kuu ya EPL.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *