
Moshi/Nairobi. Jiji la Nairobi na viunga vyake, limezizima kufuatia maelfu ya waombolezaji waliojitokeza kuupokea na kuuaga mwili wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kenya, Raila Odinga aliyefariki dunia jana Jumatano India Oktoba 15.
Ni kutokana na umati huo mkubwa, shughuli za kuuga mwili iliyokuwa ifanyike katika Bunge la Kenya zilihamishiwa Uwanja wa Kasarani huku shughuli katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), zikisimama kwa muda.
Wakati hayo yakijiri mkuu wa zamani wa Huduma ya Mawasiliano ya Habari ya Rais, Lee Njiru amesimulia namna Rais wa Kenya, Daniel Arap Moi aliyeogoza taifa hilo kati ya mwaka 1978 na 2002 alivyokataa njama ya kumuua Raila Odinga.
Mwili wa Odinga uliwasili JKIA leo saa 3:40 asubuhi kwa Shirika la Ndege la Kenya, KQ 203, ukisindikizwa na ujumbe wa viongozi 30 wa Kenya na familia yake huku Rais wa Jamhuri ya Kenya, Dk William Ruto akiongoza mapokezi ya mwili wa kiongozi huyo.
Maelfu ya wananchi walifurika katika uwanja huo wa ndege na kulazimisha Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Kenya (KAA), kusitisha shughuli uwanjani hapo kuanzia saa 4:26 asubuhi hadi saa 6:26 mchana kwa sababu za kiusalama.
“Hatua hii muhimu ni kuwezesha operesheni iliyoimarishwa ya kukagua upya usalama kufuatia kuwasili kwa mabaki ya Rais Odinga,”inaeleza taarifa rasmi iliyotolewa na Kaimu Mtendaji mkuu wa KAA, Dk Mohamud Gadi.
“Usalama wa abiria wetu, wafanyakazi na watumiaji wote wa uwanja wa ndege ndio kipaumbele chetu cha juu na hatua hii ni sehemu ya dhamira yetu isiyoyumba ya kudumisha viwango vya juu zaidi vya usalama,”anasisitiza Dk Gadi.
KAA iliwataka abiria walio na safari za ndege zilizoratibiwa katika kipindi hicho kuwasiliana na mashirika yao ya ndege moja kwa moja ili kupata taarifa zaidi kuhusu marekebisho yanayoweza kufanywa katika ratiba za safari zao.
Misafara ya magari, pikipiki na ya wafuasi wa mwanasiasa huyo ambaye walizoea kumuita “Baba” wakitembea kwa miguu ulionekana kuanzia JKIA hadi Uwanja wa Kasarani na mwili uliwasili uwanjani hapo saa 8:35 mchana.
Uwanja huo unakadiriwa kuwa na uwezo wa kupokea mashabiki kati ya 40,000 hadi 60,000 kulingana na shughuli inayofanyika na kwa muonekano wa jana, uwanja huo ulionekana kuelemewa na maelfu kwa mamia ya waombolezaji.
Polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi ilipofika 9:10 mchana kutokana na wingi wa watu waliokuwa wakipiga kelele, kulia na wengine wakileta vurugu hali iliyowalazimu maofisa usalama kutumia vilipuzi kuwatawanya.
Simulizi ya jaribio la mauaji
Akizungumza na gazeti la Daily Nation la Kenya, Njiru ambaye ni mwanahabari mkongwe wa Kenya anasema miongoni mwa kumbukumbu zake nyingi, ni namna Rais Moi alivyokataa pendekezo la ofisa mkuu wa usalama la kumuua Odinga.
“Mzee Moi aliwahi kuniambia ofisa mmoja mkuu wa usalama alimjia na kumwambia, “mheshimiwa kwa nini mtu huyu (Raila) anakupa shida nyingi? Nipe ruhusa tumtoe (kuua). Lakini mzee akamtazama, akatikisa kichwa na kusema Hapana.”
Njiru ananyamaza kwa muda, akiruhusu uzito wa maneno kutulia kisha akasema, “ndiyo. Baadhi ya watu ndani ya utawala wa Moi walitaka Raila aondolewe.”
Kwa mujibu wa Njiru, uamuzi huo ulidhihirisha ukomavu wa kisiasa wa Rais Moi na jukumu kuu la Odinga katika demokrasia ya Kenya.
Moi alifariki dunia Februari 4, 2020 akiwa na umri wa miaka 95 na kuzikwa kwa heshima kubwa nchini humo.
“Raila alikuwa sehemu muhimu katika medani za kisiasa za Kenya. Ni mtu ambaye alipinga mamlaka, alizua mjadala, na kusukuma nchi hii kubadilika,” anasema.
Kuhusu tangazo la kifo cha Odinga ambacho kilitangazwa na Rais Ruto, alisema, “ilikuwa ya kutatanisha kwa sababu tangu mwanzo hakuna mtu aliyekuwa wazi kuhusu hali ya afya ya Raila.
“Watu hawakuwa tayari kwa tukio hili la kitaifa. Ilipothibitishwa hatimaye, nilikumbuka mauaji ya Julius Caesar na maneno ya Mark Antony ‘Why cometh such other? (Kwa nini huja vile vingine),” anasema mwanahabari huyo.
“Hivyo ndivyo mamilioni ya Wakenya watakavyouliza. Raila hakuwa na mbadala.”
Kwa mtizamo wake, kifo cha Odinga kinaweza kuzua msukosuko wa kisiasa.
“Hivi Raila kaondoka, utapeli wa kisiasa wa nchi hii utabadilika sana. Alikuwa nguzo. Iwe ulimpenda au humpendi, ilibidi uamue. Kabla ya 2027 na kuendelea, Kenya itaona mabadiliko katika jinsi siasa zitakavyoendeshwa,” anasema.
Uhusiano wa Njiru na Odinga ulikuwa ni mkubwa kutokana na wawili kufanya kazi kwa karibu wakati waziri mkuu huyo wa zamani alipokuwa katibu mkuu wa Chama cha Kenya African National Union (KANU) chini ya utawala wa Moi.