Shinyanga. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Shinyanga limekuja na suluhisho la kudumu kwa changamoto ya umeme mdogo (low voltage) inayowakabili watumiaji wakubwa wa nishati hiyo mkoani humo.

Changamoto hiyo ilikuwa inasababisha uharibifu wa mitambo na kusababisha hasara katika uzalishaji.

Wakizungumza leo Oktoba 16, 2025 katika mkutano wa wateja wakubwa wa umeme uliofanyika mjini Shinyanga, baadhi ya wawakilishi wa wateja hao akiwemo Clarence Haule, amesema changamoto ya umeme mdogo imekuwa ikisababisha uharibifu wa mitambo na hasara katika uzalishaji.

Mwakilishi mwingine Dominick Kasinge amepongeza juhudi za Serikali kuhakikisha changamoto hiyo inapatiwa ufumbuzi,

“Kwa niaba ya wenzangu naishukuru Serikali kwa kuja na suluhu ya changamoto hii, tuna imani itakuwa ndio mwisho wa uharibifu wa mitambo na uzalishaji utaongezeka,” amesema Kasinge.

Meneja wa Tanesco Kanda ya Magharibi, Mhandisi Richard Swai akizungumza na wateja wakubwa wa umeme Shinyanga.

Naye, Mhandisi Mwandamizi wa Tanesco, Antony Tarimo amesema suluhisho hilo linahusisha utekelezaji wa mradi wa uzalishaji wa megawati 150 kupitia nishati ya jua,

“Suluhisho hilo linahusisha utekelezaji wa mradi wa uzalishaji wa megawati 150 kupitia nishati ya jua pamoja na ufungaji wa kifaa cha kisasa cha kudhibiti mabadiliko ya nguvu za umeme (Automatic Voltage Regulator). Pia hatua hizo ni sehemu ya mkakati wa Serikali kupitia Tanesco kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wawekezaji, viwanda, migodi na taasisi kubwa zinazotumia umeme mwingi.”

Aidha, Meneja wa Kanda ya Magharibi, Mhandisi Richard Swai amebainisha kuwa shirika hilo  linaendelea kuboresha miundombinu ya usambazaji na kuongeza uwezo wa mitambo, ili kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukuza uwekezaji na uchumi wa viwanda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *