Mwanza. Pamba Jiji ya Mwanza ni miongoni mwa timu tatu ambazo hazijapata ushindi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, ambapo kesho itakuwa na kibarua kizito cha kuhakikisha inatafuta ushindi wa kwanza.
Timu hiyo, Fountain Gate na TRA United ni timu tatu ambazo hazijaonja ushindi msimu huu baada ya kucheza michezo mitatu, huku TRA ikiwa imecheza mechi mbili.
Pamba inakamata nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na alama mbili baada ya kucheza michezo mitatu na kuambulia sare mbili na kupoteza mmoja, huku ikifunga bao moja pekee na kuruhusu manne.

Kesho Ijumaa Oktoba 17, 2025 Pamba Jiji itakuwa na mtihani mwingine wa kusaka ushindi wa kwanza msimu huu itakapowakaribisha maafande wa Mashujaa FC ya Kigoma katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kuanzia saa 8:00 mchana.
Mchezo huo ni wa tatu kwa timu hizo kukutana tangu Pamba Jiji ilipopanda Ligi Kuu msimu uliopita, ambapo katika mechi mbili za ligi walizokutana Mashujaa ameshinda moja (2-0) katika Uwanja wa Lake Tanganyika, na sare moja (2-2) kwenye dimba la CCM Kirumba.
Akieleza maandalizi ya kikosi chake kuelekea mchezo huo, Kocha Mkuu wa Pamba Jiji, Francis Baraza amesema maandalizi yote yamekamilika na wachezaji wake wako tayari, huku akisisitiza kwamba hawana visingizio vyovyote vya kutopata ushindi kwani wanacheza nyumbani mbele ya mashabiki wao.
”Timu mpaka sasa iko vizuri maandalizi yameshakwisha jambo la kungoja tu mchezo wa kesho na kuona vijana watafanya vizuri. Wachezaji wangu wako tayari najua utakuwa mchezo mgumu lakini tuna faida tunacheza nyumbani na hatuna kisingizio chochote cha kutopata pointi tatu,” amesema Baraza.
Ameongeza kuwa; “Kwahiyo ni juhudi ya wachezaji kama wataweza kubeba kile tulichokifanya mazoezini kama watayafuata maelekezo yetu basi bila shaka najua tutatoka na ushindi kesho.”

Kiungo wa Pamba Jiji, Abdallah Hamis
amesema katika mechi tatu zilizopita wameshaonja ladha ya kufungwa na kutoa sare, hivyo hawahitaji kitu kingine chochote zaidi ya kushinda na kuwapa furaha mashabiki wa Mwanza.
”Keso hakuna mambo mengi ni mchezo muhimu sana tunahitaji kupata ushindi, sisi wachezaji hatuwezi kuwa na maana kama hatumsikilizi mwalimu, hivyo, tunahitaji pointi tatu hatuhitaji mambo mengi,” amesema Hamis.
Naye, Kocha Mkuu wa Mashujaa FC, Salum Mayanga amesema wamefanya mazoezi ya mwisho jana na leo asubuhi kwenye uwanja wa mechi na wametumia muda huo kusahihisha makosa yaliyotokea katika mchezo wa mwisho dhidi ya Singida Black Stars waliopoteza kwa bao 1-0.
”Mategemeo yangu ni kwamba kesho tutacheza vizuri na kupata ushindi, tunajua Pamba wanacheza nyumbani na tumejaribu kuwafuatilia, tumeandaa mpango ambao utatusaida kuwakabili,” amesema Mayanga.
Ameongeza kuwa; “Tutacheza kwa uhangalifu zaidi na kuwa na tahadhari katika kujilinda. Malengo yetu ni kufanya vizuri kwenye ligi kuu na kumaliza katika nafasi iliyo salama zaidi, kwahiyo tunahitaji kushinda mechi nyingi iwezekanavyo.”