
Dar es Salaam. Serikali imeanza kutekeleza ahadi yake ya kuiimarisha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) baada ya kukabidhi magari 140 kwa taasisi hiyo, ili kuongeza ufanisi katika usajili na utambuzi wa watu nchini.
Hatua hiyo imetajwa kuwa miongoni mwa mikakati ya Serikali kuboresha mifumo ya utambuzi wa raia na kutekeleza mpango wa Jamii Namba.
Kwa miaka mingi, Nida imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya uhaba wa vitendea kazi, hususan magari ya kufikia wananchi waliopo katika maeneo ya vijijini na pembezoni.
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2022/2023 ilibainisha ucheleweshaji wa vitambulisho na ukosefu wa miundombinu uliathiri zaidi ya asilimia 30 ya waombaji.
Hali hiyo, ilichangia idadi kubwa ya Watanzania kukosa huduma muhimu kama kufungua akaunti benki, kupata huduma za Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), huduma za simu na hata kusafiri nje ya nchi.
Makabidhiano ya magari hayo, yamefanyika jijini Dar es Salaam leo Alhamisi Oktoba 16, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa Nida, James Kaji kwa Maofisa Usajili wa Wilaya za Uvinza, Sumbawanga, Mpanda na Karagwe.
Amesema magari hayo yananunuliwa kwa fedha za Serikali kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025.
“Tunashukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kuimarisha Nida. Serikali imetumia fedha nyingi, hivyo ni wajibu wetu kuyatunza na kuyatumia kama ilivyokusudiwa ili kuleta tija kwa Taifa,” amesema.
Kaji amesisitiza kila ofisi ya Nida ya wilaya itapatiwa gari moja, jambo litakalorahisisha utoaji huduma za usajili, usafirishaji wa vifaa, ufuatiliaji wa taarifa na uhamasishaji wa wananchi.
Amesema hadi sasa, magari 17 yameshakabidhiwa na yamesambazwa katika mikoa mbalimbali, huku mengine yakitarajiwa kuwasili kwa awamu kadri taratibu za manunuzi zinavyokamilika.
Mpango huo pia unaendana na utekelezaji wa dhana ya Jamii Namba iliyoanzishwa rasmi mwaka 2023, inayolenga kutoa namba ya utambulisho wa Taifa kwa mtoto mara tu anapozaliwa badala ya kusubiri afikishe miaka 18.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, mpango huo utasaidia kuondoa changamoto ya utambuzi wa raia na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii na kiuchumi.
Mathalan, takwimu za Nida zinabainisha kufikia Juni 2024, ni asilimia 64 tu ya Watanzania waliokuwa wamesajiliwa na kupata vitambulisho vya Taifa, huku zaidi ya watu milioni 15 hawakuwa wamepata huduma hiyo.
Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni alinukuliwa bungeni Aprili 2024 akisema, Serikali imetenga zaidi ya Sh50 bilioni kwa ajili ya kuimarisha mifumo, kuongeza watumishi, kununua vifaa na magari kwa Nida.
Magari hayo yanatarajiwa kupunguza muda wa usajili na uchukuaji wa alama za vidole, hususan katika mikoa yenye maeneo makubwa ya kijiji kama Ruvuma, Tabora, Katavi na Kigoma.
Awali, maofisa wa Nida walilazimika kupata usafiri wa kukodi au kushirikiana na ofisi za halmashauri, hali iliyochelewesha huduma na kuongeza gharama.
Serikali pia inalenga kuunganisha taarifa za Nida na mifumo mingine ya kitaifa kama Wakala wa Usajili wa Vizazi na Vifo (Rita), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Daftari la Wapigakura na benki.
Kwa mujibu wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa 2021/2026, mfumo thabiti wa utambulisho wa taifa ni msingi wa uchumi wa kidijitali na utawala bora.
Kupitia uwekezaji huo, Serikali itaondoa malalamiko ya muda mrefu dhidi ya Nida na kuweka msingi madhubuti wa uchumi wa kidijitali, usalama wa taifa na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.