
Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Tunisia wamesisitiza kuwa, kulitatua suala la Palestina kunahitaji kukomeshwa kukaliwa kwa mabavu na kutekelezwa haki ya kujitawala wananchi wa Palestina.
Seyyed Abbas Araqchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Mohamed Ali Al-Nafti, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia wamesisitiza hayo pambizoni mwa Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM huko Kampala, mji mkuu wa Uganda na kujadili masuala mbalimbali.
Katika mazungumzo hayo, pande hizo mbili zilipitia matukio ya hivi punde katika mahusiano baina ya nchi hizo mbili, ikiwa ni pamoja na maandalizi yaliyofanywa ili kufanya mkutano wa Tume ya Pamoja ya Uchumi, na kusisitiza dhamira ya pamoja ya nchi hizo mbili ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano katika nyanja zoe zenye maslahi.
Vile vile walibadilishana mawazo kuhusu matukio ya eneo la Magharibi mwa Asia na kukaliwa kwa mabavu Palestina kwa kuzingatia makubaliano yaliyofikiwa nchini Misri ya kusimamisha mauaji ya kimbari huko Ghza, na kusisitiza wajibu wa wadhamini wa kuuzuia utawala wa Kizayuni kukiuka mapatano yake.
Araghchi akiwa Kampala pia alikutana na Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni na kubainisha umuhimu mkubwa wa Iran katika kuimarisha uhusiano na Afrika na kusisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kupanua uhusiano na Uganda katika nyanja za kiuchumi, kilimo na biashara.