Mashambulio ya utawala ghasibu wa Israel katika Ukanda wa Gaza yamesababisha kuibuka migogoro 15 ya kimsingi kwa wakazi wa eneo hilo.

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, mashambulio ya utawala wa Israel dhidi ya Gaza yamesababisha kuibuka migogoro 15 ya kimsingi kwa wakazi wa eneo hilo, ambayo yametokea ndani ya fremu ya mauaji ya kimbari ambayo hayajawahi kushuhudiwa na ya kimfumo, ambayo lengo lake limekuwa ni kutoa mashinikizo kwa wananchi, kuwalazimisha Hamas kusalimu amri na kuwaondoa kwa nguvu Wapalestina.

Mgogoro wa kwanza ni mauaji ya halaiki ambayo yamesababisha zaidi ya watu 76,000 kuuawa au kutoweka na karibu 169,000 kujeruhiwa. Wengi wa waliojeruhiwa wameachwa na vilema vya kudumu.

Mgogoro wa pili ni kunyimwa fursa ya kupata chakula, maji, na vitu muhimu vya maisha. Utawala wa Kizayuni umepiga marufuku uingiaji wa vyakula, dawa, mafuta na vifaa vya ujenzi, na watu wanakabiliwa na matatizo makubwa katika kukidhi mahitaji yao ya kimsingi.

Shida ya tatu ni kuporomoka kwa huduma za afya na uhaba mkubwa wa dawa. Hospitali zimefungwa na wagonjwa hawapati hata dawa rahisi.

Mamia ya shule za Gaza zimebomolewa kabisa

Mgogoro wa nne ni uharibifu mkubwa wa nyumba na makazi ya kulazimishwa ya watu katika mahema yasiyoweza kukaliwa. Mgogoro wa tano ni marufuku ya kuingia kwa bidhaa za kimsingi kama vile nguo, viatu na mafuta, na kutatiza  maisha ya kila siku.

Mgogoro wa sita ni wa usafiri unaosababishwa na uharibifu wa magari na ukosefu wa mafuta, ambao umewalazimu watu kutumia mikokoteni na wanyama. Mgogoro wa saba ni marufuku ya kuondoka Gaza, hata kwa wagonjwa na waliojeruhiwa. Mgogoro wa nane ni kuporomoka kwa uchumi na kupoteza vyanzo vya mapato vya watu, hali ambayo imewalazimu kuuza bidhaa zao za nyumbani au kuomba msaada kutoka kwa jamaa.

Mgogoro wa tisa ni kufungwa kwa benki na ukosefu wa upatikanaji wa pesa taslimu. Mgogoro wa kumi ni ukosefu wa huduma za umma kama vile kuzoa taka na maji taka kutokana na kulenga mfumo wa serikali. Mgogoro wa kumi na moja ni udhaifu mkubwa wa mawasiliano na mtandao, ambao umetatiza uhusiano wa familia na biashara kwa ujumla.

Mgogoro wa kumi na mbili ni kusitishwa kabisa kwa elimu katika shule na vyuo vikuu, jambo ambalo limekuwa na athari mbaya kwa kiwango cha taaluma ya wanafunzi. Mgogoro wa kumi na tatu ni kukatika kabisa kwa umeme na kutegemea jenereta chache. Mgogoro wa kumi na nne ni wizi wa misaada ya kibinadamu unaofanywa na vikundi vilivyoandaliwa vinavyoungwa mkono na wavamizi.

Mgogoro wa kumi na tano ni mgawanyiko wa Gaza katika sehemu za kaskazini na kusini na kukata uhusiano kati ya familia.

Msururu huu wa migogoro unaakisi hali mbaya ya kibinadamu huko Gaza na matokeo yaliyoenea ya vita na mzingiro katika maisha ya kila siku ya watu wa eneo hili.

Maji ni miongoni mwa huduma muhimu ambazo upatikanaji wake umekuwa shida huko Gaza

Hivi sasa licha ya kuanza kutekelezwa makubaliano ya usitishaji vita na wakimbizi wa Kipalestina kuendelea kurejea katika makazi yao, lakini Wapalestina hao wanakabiliwa na hali mbaya mno ya maisha kutokana na kupoteza suhula zao za maisha kama nyumba na kadhalika.

Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana asasi mbalimbali za utoaji misaada zinasisitiza juu ya kurahishwa na kutekelezwa kikamilifu usitishaji vita na wakati huo huo, kupelekwa haraka misaada ya kibinadamu katika Uukanda wa Gaza ili kukidhi mahitaji ya lazima ya wakazi wa Ukanda huo.

Kwa mujibu wa taasisi hizo za kimataifa, makubaliano yanayolega lega ya usitishaji vita huko Gaza, yaliyofikiwa chini ya mpango wa Rais wa Marekani Donald Trump, yanahitaji kuona njia zikifunguliwa ili misaada iweze kumiminwa kwenye eneo hilo linaloatilika kwa njaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *