
Mstaafu wetu anashukuru alianza kazi miaka ilee ambayo mashirika na kampuni za Siri-kali na binafsi zilikuwa zinatafuta waajiriwa wanapomaliza masomo shule za sekondari tofauti na sasa waajiriwa hulazimika kuisaka ajira kwa kurunzi, na bado hawaioni!
Mstaafu wetu anazungumzia zile enzi tulizokuwa na chuo kikuu kimoja tu, nchi nzima na watu huingia hapo kwa mahesabu, hivyo mashirika na kampuni zote hulazimika kuandika barua Wizara ya Elimu kuomba itumiwe idadi ya wanafunzi inayohitaji waliomaliza kidato na nne na sita ambao hawakupata nafasi ya kujiunga na vyuo vichache vilivyokuwepo ili waajiriwe.
Hii ina maana kuwa baada ya mwaka mmoja tu kumaliza sekondari tayari ulikuwa ofisa wa benki, bandari, reli, posta na simu.
Tofauti na sasa, unaweza kumaliza kusoma kwenye moja ya rundo la vyuo vikuu tulivyo navyo na miaka mitatu baadaye ukawa bado unaitafuta ajira kwa tochi, baraka ya kununua na kumaliza tu betri za tochi hiyo ukitafuta ajira!
Mstaafu wetu anashukuru kwamba miaka 45 iliyopita alikuwa mmoja wale waliopata ajira waliomaliza sekondari na anashukuru zaidi aliajiriwa enzi zilee ambazo mashirika na kampuni ndizo zilikuwa zikitafuta waajiriwa na sio kwa tochi.
Tofauti na siku hizi, vyeti na barua za maombi ya kazi huishia kupauka mikononi vijana wanaohangaika barabarani kuisaka ajira!
Mstaafu anakiri mshahara wake wa kwanza kabisa pale Bomani ofisi ya mkuu wa Wilaya ya Kigoma, ulikuwa ni Shilingi 380! Huku ukikatwa nadhani Shilingi 175 kwenda kibubu cha akiba ya wafanyakazi cha NPF(National Provident Fund) kilichokuwa pekee enzi hizo, halafu shilingi nane na senti hamsini kwenda Paye (Pay As You Earn ) ‘Lipa Upatacho,’ ili tujenge shule msome bure!
Kuanzia miaka ya 2010 waheshimiwa wakaminya kitufe cha ‘fast foward’ na mambo yakaanza kwenda sege mnege, na keki ya Taifa waliyojitahidi sana ‘kuipika’ wastaafu’ wa nchi ikaanza kuunguzwa kwa makusudi huku watu ambao hawajui ‘kupika’ keki hiyo ya Taifa wajikatia vipande vinono huku Mstaafu aliyehusika sana ‘kuipika’ akianza kuambulia harufu tu!
Ilianzia kule kwenye akiba yetu ya uzeeni, waheshimiwa wetu, bila kutuuliza sisi wenye ela zetu, wakajiongeza na kukigeuza kibubu chetu kuwa ‘kausha damu’ ya namna fulani kwa kutumia akiba yetu kutoa mikopo mikubwa kwa watu, ikiwamo Siri – Kali yenyewe bila sisi kulipwa chochote pamoja kuwa ni hela yetu iliyotumika kutoa mikopo hiyo!
Watu wakakopa magari na kujenga madaraja na kibubu kikajenga ‘vikwangua anga’ vya kukodisha na kuuza huku mstaafu mwenye hela zake zinazotumika kwenye mikopo hiyo, haambulii chochote!
Wakati hata kuanzisha kibubu cha kutoa mikopo yenye riba nafuu ili kumsaidia mstaafu wetu asibamizwe na mikopo ya hizi benki za dotcom ambazo riba ya mikopo yake!
Halafu wabunge wanaosemekana kuwa wawakilishi wa wananchi wanafikia kulipwa Sh16 milioni kwa mwezi huku mstaafu wa kima cha chini ‘ aliyeipika’ keki ya Taifa akiambulia pensheni ya shilingi laki moja na elfu hamsini kwa mwezi kwa miaka 21!
Hakuna mheshimiwa ambaye anajisumbua kutaka kujua mstaafu anatumia muujiza gani kuweza kuishi kwa shilingi laki moja nusu kwa mwezi, maana wahusika wenyewe wako bize kula urefu wa kamba zao, mradi hawapigi kelele!
Ni mwakilishi huyu huyu ambaye baada ya miaka mitano ya kuunga mkono hoja, analipwa kiinua mgongo kweli cha shilingi…mama wee!…milioni mia nne, wakati mstaafu wetu aliyeijenga nchi kwa ajira ya miaka 40 anapata ‘kipindisha mgongo’ cha milioni 40!
Naam, yale yale ya mcheza mpira wa miguu kulipwa Sh5 milioni kwa kufunga goli kwenye mechi ya dakika.
Mstaafu wa kima cha chini akiishia kupata Shilingi laki moja na elfu hamsini kwa siku thelathini!
Mstaafu wetu asilaumiwe asiposikia harufu ya keki ya Taifa. Anahisi matumizi na matanuaji haya yamefanya pua yake iote sugu, pamoja na Kibubu kudai kuwa kitampa Sh5.5 milioni akifariki na kuwa mkazi wa kudumu wa Kinondoni!